Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Joyce Kyando akitoa elimu kuhusu namba tano muhimu za afya kwa wanariadha katika mdahalo wa afya wakati wa mbio za capital city half marathon zilizofanyika leo katika viwanja vya Chimwaga vilivyopo jijini Dodoma.
Afisa uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed Wamara akimpima kiwango cha sukari kwenye damu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Samwel Lazaro wakati wa mbio za capital city half marathon zilizofanyika leo katika viwanja vya Chimwaga vilivyopo jijini Dodoma.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Joyce Kyando, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Samwel Lazaro, Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Capital City Half Marathon Nsolo Mlozi na Miss Universe Tanzania 2026 Queen Elizabeth wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa mdahalo wa afya uliofanyika katika viwanja vya Chimwaga vilivyopo jijini Dodoma.
Picha na JKCI
……………
Na Mwandishi Maalum Dodoma
01/11/2026 Wanariadha nchini wahimizwa kupima afya zao na kufahamu viashiria muhimu vya mwili kabla ya kushiriki katika mashindano mbalimbali ili waweze kubaini mapema changamoto zinazoweza kuhatarisha maisha yao wakati wanakimbia.
Wito huo umetolewa leo na daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Joyce Kyando katika mdahalo uliofanyika wakati wa ufunguzi wa mbio za Capital City Half Marathon katika viwanja vya Chimwaga vilivyopo jijini Dodoma.
Dkt. Joyce alisema wanariadha wanapaswa kufahamu viashiria muhimu vya afya kwani wanaweza kujihisi mwenye afya njema lakini vipimo vikabaini mabadiliko yanayohitaji ufuatiliaji au ushauri wa kitaalamu.
“Ni muhimu kujua namba zetu za afya ikiwemo shinikizo la damu, sukari kwenye damu, mafuta mwilini na uwiano wa uzito na urefu (BMI) vipimo hivi vinatusaidia kufahamu hali ya mwili na kubaini mapema kama kuna changamoto zinazohitaji ufuatiliaji”, alisema Dkt. Joyce.
Dkt. Joyce alisema kufanya mazoezi mara kwa mara ni tabia muhimu katika kuimarisha afya ya mwili na kupunguza hatari inayoweza kumsababishia mtu kupata magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo.
“Magonjwa yasiyoambukiza yana gharama kubwa za matibabu, hivyo ni muhimu kujali afya zetu na kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara”, alisema Dkt. Joyce.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Samwel Lazaro alisema kutofanya mazoezi ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuongezeka kwa hatari ya magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo kisukari na shinikizo la damu.
“Ni muhimu washiriki wa mbio za Capital City Half Marathon wafahamu namba zao za afya kabla ya kushiriki marathon ndiyo maana huduma za kupima uzito, urefu, shinikizo la damu na sukari zinatolewa hapa ili wanariadha wajue hali zao na kupata ushauri unaofaa”, alisema Dkt. Lazaro.
Dkt. Lazaro aliongeza kuwa wanamichezo wanapaswa kuendeleza tabia ya kufanya mazoezi na kufuatilia afya zao hata baada ya mashindano ili kupunguza hatari ya magonjwa yanayohusiana na kutokufanya mazoezi.
“Tunawahimiza wananchi kuendelea kufanya mazoezi na kutumia fursa za uchunguzi wa afya zinazotolewa, kufahamu hali ya mwili na kupata ushauri wa wataalamu ni hatua muhimu katika kujilinda na magonjwa yasiyoambukiza”, alisema Dkt. Lazaro.
Ushiriki wa JKCI katika mbio za Capital City Half Marathon ni muendelezo wa kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuzuia magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza kupitia elimu, uchunguzi wa afya na kusogeza huduma karibu na wananchi.
