Na Silivia Amandius
Bukoba.
Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Faris Buruhani, ametoa wito kwa viongozi wa chama hicho kuhakikisha wanasimamia na kutetea maslahi ya vijana katika maeneo yao, akisisitiza kuwa viongozi watakaoshindwa kutekeleza wajibu huo hawataendelea kulindwa na nafasi zao za uongozi.
Faris ameyasema hayo wakati akizungumza na wanakagera katika mkitano wa mapokezi uliofanyika katika viwanja vya shule ya MSINGI kashai manispaa ya bukoba ameeleza kuwa ana imani kubwa na vijana wa Tanzania na kwamba kiu ya Rais ni kuona taasisi hiyo ikirejea katika nafasi yake ya msingi ya kuwaunganisha vijana na kuwashirikisha katika maamuzi na michakato mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza kuhusu safari yake ya uongozi, Faris ameishukuru jamii ya Katoro kwa malezi mazuri aliyoyapata, akieleza kuwa mwaka 2022 alipata nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kagera.
Ameishukuru jamii hiyo pamoja na wajumbe na viongozi mbalimbali kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote cha uongozi wake, hususani wakati wa kuanzisha vikundi na shughuli za kuwawezesha vijana.
Amesisitiza kuwa msingi wa kwanza wa kuimarisha taasisi hiyo ni vijana wote kuungana na kuwa na mshikamano kama chama kimoja, huku akieleza kuwa vijana wanapaswa kushirikishwa katika maamuzi na michakato ya pamoja inayohusu maendeleo yao, pamoja na kusimamiwa katika masuala ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, amewataka viongozi wa UVCCM kwenda kusimamia kwa nguvu maslahi ya vijana, akionya kuwa kiongozi atakayeshindwa kutimiza wajibu huo atatafutiwa njia ya kuondoka katika nafasi yake. Amesisitiza kuwa nafasi za uongozi hazipaswi kuwa kinga ya kutowajibika, bali ni dhamana ya kuwatumikia wananchi.
Katika hatua nyingine, Faris amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa uadilifu na kuacha kuwakwaza wananchi wanapotekeleza shughuli zao za kujipatia kipato. Amewataka maafisa wenye dhamana kuacha vitendo vya udokozi wa kahawa za wananchi na kusimamia majukumu yao kwa kuzingatia sheria na haki.
Amesema taasisi hiyo haitakuwa sehemu ya kuwatetea watumishi wanaotumia vibaya mamlaka yao, bali itasimamia haki za wananchi na kuhakikisha kuwa hakuna anayewanyanyasa vijana au wananchi wengine katika maeneo yao ya kazi.
Akizungumzia sekta ya usafirishaji, ameeleza kuwa vijana hawapaswi kusumbuliwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), bali wanahitaji elimu na uelewa wa sheria na taratibu za usafiri ili waweze kutekeleza shughuli zao kwa amani.
Amesisitiza kuwa chama hicho hakitakuwa sehemu ya kuchochea migogoro kati ya CCM na wananchi, bali kitahakikisha heshima ya chama inalindwa kwa kutatua changamoto kwa njia sahihi.
Farisi pia ameipongeza Serikali kwa juhudi za kuboresha miundombinu, ikiwemo ujenzi wa barabara, madaraja na kuboresha huduma za elimu kupitia vyuo na taasisi za elimu katika maeneo mbalimbali na kuwaasa watumishi wa umma kutowakwamisha wananchi katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.
Ameongeza kuwa UVCCM si jumuiya ya uoga, hivyo amewataka viongozi wake kusimama imara, kutetea haki na maslahi ya vijana na kuhakikisha kuwa changamoto zinazowakabili zinapatiwa ufumbuzi.
Akihitimisha, Faris amesisitiza kuwa hatabadilika kutokana na nafasi yake mpya, akiahidi kuendelea kuwatumikia wananchi na vijana kwa uadilifu na kuhakikisha kuwa maslahi yao yanapewa kipaumbele.
Amesema kuwa dhamira yake ni kutekeleza majukumu ya uongozi kwa vitendo, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kukumbuka kuwa nafasi walizonazo ni dhamana ya kuwatumikia wananchi, si kujinufaisha binafsi

