Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewakaribisha wawekezaji wa Korea Kusini kuwekeza Zanzibar katika sekta mbalimbali za kiuchumi, huku akiwahimiza kushirikiana na wafanyabiashara wa ndani ili kuongeza mitaji, kuleta teknolojia mpya, kukuza biashara.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 30 Oktoba 2026, katika hafla ya chakula cha jioni kilichoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea (Kusini), kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Korea Kusini, iliyofanyika katika Hoteli ya Grand Hyatt, jijini Seoul, Korea Kusini.

Amesema Zanzibar ina fursa nyingi za uwekezaji, hususan katika sekta za Uchumi wa Buluu, utalii, bandari, usafirishaji na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, ambazo zimepewa kipaumbele katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050.

Dkt. Mwinyi amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kupitia sheria na kanuni zinazolinda maslahi ya wawekezaji, pamoja na kuimarisha huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), ili kurahisisha uanzishaji na uendeshaji wa miradi ya uwekezaji nchini.

Ameongeza kuwa Zanzibar ina nafasi nzuri ya kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji kutokana na eneo lake la kimkakati linalounganisha masoko ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, pamoja na fursa zinazotokana na Soko Huru la Biashara la Bara la Afrika.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza wafanyabiashara na wawekezaji wa Korea Kusini kuanzisha ubia na kampuni za Zanzibar, akieleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuunganisha uzoefu, teknolojia na mitaji kutoka Korea Kusini na fursa zilizopo Zanzibar, kwa manufaa ya pande zote mbili.

Hafla hiyo imehudhuriwa na wawakilishi wa Serikali ya Korea Kusini, wanadiplomasia, viongozi wa taasisi za fedha, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka sekta mbalimbali.

Rais Dkt. Mwinyi amekamilisha ziara yake nchini Korea Kusini, iliyohusisha mikutano ya uwekezaji na biashara jijini Seoul, ziara za viwanda na miradi jijini Yeosu, ushiriki katika Mkutano wa ITOP visiwani Jeju, pamoja na mazungumzo na makampuni ya Korea kuhusu fursa za miradi ya kimkakati Zanzibar.