Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Urusi waendelee kuitangaza vyema nchi na kuongeza juhudi za kutafuta fursa za masoko kwa bidhaa za Tanzania nchini humo.

Ameyasena hayo leo Oktoba 30, 2026, wakati akizungumza na watumishi wa Ubalozi huo ulioko jijini Moscow na kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuiwakilisha vema Tanzania nchini humo.

 Sambamba na hayo, Mheshimiwa Dkt Mwigulu amebainisha kuwa hivi sasa nchi imekuwa na uzalishaji wa mazao wa ziada unaohitaji masoko ya uhakika.

“Bado tunahitaji masoko ya bidhaa zetu. Tumekuwa na uzalishaji wa mazao wa ziada nchini, hivyo tumieni fursa hii kutengeneza masoko katika miji mingine kwa maana nchi hii ni kubwa sana. Kadhalika, endeleeni kufuatilia fursa zilizopo katika sekta ya elimu, jambo ambalo pia limejitokeza kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka watumishi hao wafuatilie na kusimamia utekelezaji wa maagizo yote yaliyotokana na ziara ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini Urusi, iliyofanyika Juni, mwaka huu.

Awali, Dkt. Mwigulu alitembelea duka la AZBUKA VKUSA linalouza bidhaa kutoka Tanzania, jijini Moscow.