NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, ameiomba Serikali kuongeza bajeti ya ujenzi na ukarabati wa barabara katika jimbo hilo ili kukabiliana na hali mbaya ya miundombinu inayotokana na kasi ya ukuaji wa mji huo.
Ngajilo amesema licha ya Serikali kuendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara, bado kuna barabara nyingi za mitaa ambazo hazipitiki vizuri, hali inayoweza kuathiri shughuli za biashara, usafiri na maendeleo ya wananchi.
Akizungumza bungeni wakati akiuliza swali la nyongeza, mbunge huyo ameishukuru Serikali kwa jitihada za ujenzi wa barabara, lakini akasisitiza umuhimu wa kuongeza fedha za bajeti ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kutokana na kupanuka kwa mji wa Iringa.
Amezitaja baadhi ya barabara zinazohitaji kujengwa au kufanyiwa ukarabati kuwa ni za Kitasengwa–Mkoga, Nduli, Kigonzile, Mafifi–Kihesa, Majitaka–Don Bosco, Bombambili–Mawelewele, Lugenge–Kwa Kabali, Makolongoni–Ilala, Kitwilu na Igumbilo.
Amesema hali ya barabara hizo inahitaji hatua za haraka za Serikali, zikiwemo kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ili kuboresha miundombinu ya usafiri na kuifanya Iringa Mjini kuwa kitovu bora cha biashara na utalii.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Festo Dugange amepongeza kazi zinazofanywa na mbunge huyo kwa maendeleo ya wananchi wa Iringa Mjini na kueleza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuboresha miundombinu katika manispaa hiyo.
Amesema wiki moja kabla ya kujibu swali hilo, alifanya ziara katika Manispaa ya Iringa akiwa pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya LAAC, ambapo walikagua miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami inayotekelezwa kupitia Awamu ya Pili ya Mradi wa Uendelezaji wa Miji Tanzania (TACTIC).
Alisema Serikali inaipongeza Iringa Mjini kwa kupata mradi huo na kwamba utekelezaji wake unaendelea, huku akisisitiza umuhimu wa kukamilisha barabara zinazotekelezwa chini ya mradi huo.
Ameeleza kuwa baadhi ya barabara zilizotajwa na Ngajilo zinahitaji kuingizwa katika mipango ya matengenezo, huku Serikali ikiwa tayari imetoa maelekezo kwa mameneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wa mikoa na wilaya kubaini barabara zinazohitaji matengenezo na kuwasilisha maombi maalumu ya fedha nje ya bajeti ya kawaida.
Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha maeneo yenye changamoto kubwa za barabara yanapatiwa ufumbuzi ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa pamoja na kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kufanya matengenezo katika barabara zenye changamoto na kuhakikisha maeneo yenye uhitaji mkubwa yanapewa kipaumbele kulingana na mahitaji yaliyopo.
