* Mfumo huo unatumia Akili Mnemba kurahisisha upatikanaji wa takwimu na kumbukumbu

*Asema Dira 2050 inatoa malengo ya kurasimisha ajira zisizo rasmi kuwa rasmi hususani kwa vijana.

Dar es salaam

Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Lazaro Londo (Mb), amezindua rasmi mfumo wa ajira kidijitali wa ukulikanao kama AMLine Workers Portal unaotumia teknolojia ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI) kuunganisha watu wanaotafuta ajira na waajiri.

Mhe.Londo amesema,Teknolojia hii ni sehemu ya juhudi za kutumia teknolojia kurahisisha upatikanaji wa fursa za ajira nchini kwa kampuni ya AMLine unaolenga kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri kupitia jukwaa moja la kidijitali, ambapo wanaotafuta ajira wanaweza kusajili taarifa zao za kitaaluma, ujuzi na uzoefu, huku waajiri wakitumia mfumo huo kutafuta wafanyakazi wenye sifa zinazokidhi mahitaji yao.

Kupitia mfumo huo, mwajiri anaweza kusimamia mahudhurio ya wafanyakazi, upangaji wa kazi na malipo, pamoja na taarifa zinazohusu michango ya kisheria. 

Aliongeza kuwa mfumo huo unalenga kupunguza muda na gharama za kuajiri, kurahisisha usimamizi wa wafanyakazi na kuongeza uwazi katika taratibu za ajira.

Aidha, mfumo huo unalenga kusaidia kurasimisha ajira zisizo rasmi, ikiwemo kazi za muda, kwa kuwezesha utunzaji wa kumbukumbu za kazi na taarifa za wafanyakazi na pia unalenga kuboresha upatikanaji wa takwimu za nguvu kazi zinazoweza kusaidia katika upangaji wa mipango ya maendeleo na kurahisisha usimamizi wa masuala ya ajira

Uzinduzi wa mfumo huu unaonesha nafasi ya teknolojia katika kuunganisha nguvu kazi na mahitaji ya soko la ajira, sambamba na Dira 2050 na ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ukiwa muhimu katika kupanua fursa za kiuchumi kwa Watanzania, hususan vijana wanaoingia katika soko la ajira.