Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), leo tarehe 28, Oktoba, 2026 imesaini makubaliano na Shirika la Kikristo la Misaada ya kibinadamu, Maendeleo na Utetezi wa Watoto (World Vision Tanzania) kwa ajili ya ushirikiano ili kuwapatia vijana wa kike na wa kiume kutoka kwenye mazingira magumu ujuzi na kupanua fursa zao za kuajiriwa na kujiajiri.

Mradi huo ujulikanao kama BLOOM utatekelezwa katika mkoa wa Dare es Salaam na utawanufaisha vijana 3500 kwa uwiano wa asilimi 60 vijana wa kike na 40 vijana wa kiume.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore na Mkurugenzi Rasimali watu na Maendeleo wa World Vision Tanzania, Dkt Gideon Cohen, katika ukumbi wa Mikutano wa Nefaland, Manzese, jijini Dar es salaam.

Makubaliano hayo yatatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano na yamelenga kuimarisha uwezo wa vyuo vya ufundi stadi kutoa mafunzo jumuishi, yenye ubora, yanayozingatia umahiri (competence-based) na yanayoendana na mahitaji halisi ya soko la ajira.Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, ushirikiano huo unaendana na mwelekeo wa maendeleo uliowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayosisitiza kujenga uchumi shindani, jumuishi na unaotegemea ujuzi, ubunifu na matumizi ya teknolojia. 

“Ili kufikia malengo hayo, ni muhimu kuwa na nguvu kazi yenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya sekta mbalimbali za Uchumi,” Amesema Kasore 

Kasore ametoa wito kwa sekta binafsi, waajiri na wadau wengine wa maendeleo kuendeleza ushirikiano na VETA ili kuwekeza katika rasilimali watu na kujenga taifa lenye vijana wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kushindana katika uchumi wa kisasa.

Amesema VETA itatekeleza wajibu wake kwa kuhakikisha vijana wanaopata fursa kupitia ushirikiano huo wanapewa mafunzo yenye ubora, yanayozingatia umahiri na mahitaji ya soko la ajira. 

“Tutaendelea kuimarisha uwezo wa wakufunzi, kuboresha mazingira ya kujifunzia, kushirikiana na waajiri na kuhakikisha mafunzo yanatoa matokeo yanayopimika katika ajira, kujiajiri na maendeleo ya vijana,” Ameongeza.Naye Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Maendeleo wa World vision, Dkt Gideon Cohen amesema ushirikiano huo ni una umuhimu mkubwa, kwani unakwenda kuboresha maisha ya vijana kwa kuwapatia juzi utakaowawezesha kupata kazi zenye staha sambamba na kunufaika na fursa za uchumi wa kidigitali, buluu na kijani ambao sasa unakuwa kwa kasi hapa nchini.

“Tunafahamu nchini Tanzania si vijana wote wanapata elimu ujuzi katika mfumo ulio rasmi na kwa wale wanaoshindwa kuendelea na elimu ya juu VETA ndicho chombo pekee kinachoweza kuwapatia ujuzi katika stadi kama vile ufundi bomba, umeme, udereva, ufundi wa magari, upishi, ushonaji na mfunzo mengine mengi ya vitendo na tunatambua miongoni mwa hizi stadi hakuna utakayosema imepitwa na wakati haihitajiki,” amesema Dkt Cohen.

Dkt Cohen ameishukuru VETA kwa kuonesha utayari wa kuendelea kufanya kazi na World Vision ili kuleta mabadiliko kwa vijana wa Kitanzania na kuwazesha kupata ujuzi utakaowawezesha kunufaika na fursa za kiuchumi nchini.