Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeendelea na zoezi la kitaifa la utoaji elimu kwa umma kuhusu Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa la Afrika Mashariki, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa kuimarisha mtangamano wa kikanda.

Akifungua zoezi hilo mkoani Mbeya, Oktoba 28, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Jumanne Sagini, amesisitiza umuhimu wa wananchi kupata uelewa sahihi kuhusu Fungamano la Kisiasa na kutumia fursa hiyo kutoa maoni yatakayochangia maandalizi ya Rasimu ya Katiba inayozingatia maslahi na matarajio yao.

Mhe. Sagini ameeleza kuwa ushirikishwaji wa wananchi ni hatua muhimu katika kuhakikisha mchakato wa Fungamano la Kisiasa unazingatia mitazamo ya makundi mbalimbali ya jamii na kuimarisha uelewa wa pamoja kuhusu mustakabali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Zoezi hilo limewakutanisha wadau kutoka Serikali ya Mkoa, viongozi wa Serikali za Wilaya, jumuiya za wafanyabiashara, taasisi za dini, mashirika ya kiraia pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii, wakiwemo vijana, wanawake na watu wa makundi maalumu.

Akiwasilisha mada kuhusu Fungamano la Kisiasa, Bw. Salehe Mubarak, ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Uandishi wa Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa, ametoa elimu kuhusu dhana, madhumuni na hatua mbalimbali za mchakato huo, ambao ni hatua ya mpito kuelekea Shirikisho la Kisiasa, iliyopitishwa na Wakuu wa Nchi za EAC mwaka 2017.

Katika mada hiyo, masuala ya msingi yanayohitaji uelewa na maoni ya wananchi ni pamoja na mgawanyo wa majukumu na mamlaka kati ya nchi wanachama na Fungamano, mfumo wa kufanya maamuzi na namna ya kuhakikisha maslahi ya wananchi yanazingatiwa katika hatua mbalimbali za mtangamano.

Aidha, washiriki wamepata fursa ya kufanya majadiliano, kuuliza maswali na kutoa maoni kuhusu masuala muhimu yanayohusu muundo wa utawala, mfumo wa kufanya maamuzi, maeneo ya ushirikiano na uhusiano kati ya Serikali za nchi wanachama na mamlaka ya Fungamano.