Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Latifa Mohammed Khamis akizungumza jambo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. Richard Muyungi wakati wa ufunguzi wa kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika tarehe 28, Oktoba 2026 Jijini Dar es Salaam kujadili maandalizi ya Tanzania kuelekea Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama Wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 31).

…..

Tanzania imeainisha vipaumbele vya kitaifa vitakavyoongoza majadiliano ya Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 31) unaotarajia kufanyika tarehe 9-20 Novemba mwaka huu nchini Uturuki.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Latifa Mohammed Khamis wakati akifungua kikao cha Makatibu Wakuu kuhusu maandalizi ya Tanzania kuelekea Mkutano wa (COP 31).

Dkt. Latifa amesema wakati wa majadiliano ya mkutano huo, Tanzania inatarajia kuwasilisha vipaumbele vinavyohusiana na fedha za tabianchi, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na upunguzaji wa uzalishaji wa gesi chafuzi.

Ametaja vipaumbele vingine kuwa ni utekelezaji wa Makubaliano ya Paris, uhamishaji wa teknolojia, kujenga uwezo, masoko ya kaboni chini ya Ibara ya 6, pamoja na hasara na uharibifu unaotokana na mabadiliko ya tabianchi.

“Ni muhimu kuhakikisha kuwa msimamo wetu unaakisi vipaumbele vya Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na mahitaji ya sekta za kilimo, maji, nishati, afya, miundombinu, misitu, mifumo ya ikolojia, bahari na uchumi wa buluu” amesema Dkt. Latifa.

Ameeleza kuwa vipaumbe hivyo vitatoa fursa kwa Tanzania kuendeleza ajenda za nishati safi, usalama wa chakula, uchumi wa buluu, uhifadhi wa mazingira, viwanda vya kijani na ushiriki wa vijana.

Ameeleza kuwa kuelekea mkutano huo ni muhimu kwa wataalamu kukamilisha mpango kazi ikihusisha maandalizi ya mikutano ya pembezoni, mikutano ya uwili na shughuli zitakazofanyika katika jengo la maonesho la Tanzania.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Kemilembe Mutasa amesema maelekezo yaliyotolewa katika kikao hicho yatawekewa mpango wa utekelezaji wenye majukumu yaliyo wazi, muda maalumu na utaratibu wa ufuatiliaji.

“Ni muhimu kwa Makatibu Wakuu kupitia matokeo ya majadiliano haya, kutoa maelekezo ya Serikali na kukubaliana kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kukamilisha maandalizi ya kitaifa kwa wakati” amesema Kemilembe.

Aidha amewataka washiriki wa mkutano huo ikiwemo Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau wengine kuimarisha ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao kwa wakati ili kufanikisha malengo ya ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la kimataifa la uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu (IUCN), Bw. Ghaamid Abdulbasat amesema Shirika hilo limeendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais katika utekelezaji wa ahadi za mikataba ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi.

Akitolea mfano amesema Shirika hilo kwa linashirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza Programu ya Urejeshaji ya kidunia (TRI) inayolenga kurejesha uoto wa asili katika ardhi iliyoharibika takribani hekta milioni 5.2 ifikapo mwaka 2030 katika mabonde ya Ruaha Mkuu na Ziwa Rukwa, katika mikoa ya Iringa, Mbeya na Rukwa.