Na mwandishi wetu, Mirerani
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imetembelea eneo la machimbo ya madini ya Tanzanite, kitalu C kinachomilikiwa kwa ubia, baina ya kampuni ya Franone Mining & Gem LTD na Serikali.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Subira Mgalu akiwaongoza wajumbe wake amepokelewa na Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining & Gem LTD Onesmo Mbise na kutoa taarifa kwa kamati hiyo.
Mbise amesema kampuni hiyo ina wafanyakazi takribani 500 na hulipa mishahara ya kuanzia shilingi 600,000 ila awali walikuwa wanalipa kina cha chini shilingi 350,000 na hutumia shilingi bilioni 1 kwa mwezi katika uendeshaji.
Amesema awali kulikuwa na uzalishaji wakutosha wa madini ya Tanzanite ila hivi sasa umepungua na wanapambana kufanya kazi ili kufanikisha uzalishaji.
“Pamoja na hayo tunaomba Serikali ifanikishe upatikanaji wa maji kule kwa wachimbaji wadogo ili kuondoa vumbi migodini kuepusha magonjwa ila sisi tunaendelea na kazi tukiwa na uhakika wa maji kwani kuna visima tunatumia,” amesema Mbise.
Mmoja wa wataalam wa jiolojia ya miamba wa kampuni hiyo, Faustine Ruta amesema madini ya Tanzanite yaligunduliwa mwaka 1967 na mtu aitwaye Ally Juu ya Watu.
Ruta amesema madini ya Tanzanite yenye zaidi ya miaka 60 tangu yagunduliwe yakiwa yanapatikana kupitia milima ya Lelatema.
Mmoja kati ya wajumbe wa kamati hiyo Neto Kapalata ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Nzega vijijini amesema uchimbaji wa madini ya vito ya Tanzanite ni tofauti na uchimbaji wa madini ya dhahabu.
“Uchimbaji wa Tanzanite ni tofauti na dhahabu kwani inachimbwa kwa kufuata ulalo unaoelekea kwenye uzalishaji ni jiwe la kipekee lenye kuangaliwa kwa thamani ya uzuri wa rangi, uzito, ubora na umbo,” amesema Kapalata.
Amesema hata mlipuaji baruti anapaswa kuchukua tahadhari anapofika kwenye uzalishaji kwani anaweza kuisambaratisha tofauti na dhahabu ambayo inaumbwa kupitia mchakato.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu ameipongeza kampuni ya Franone Mining kwa namna inavyofanya shughuli zao za uchimbaji.
Mgalu ameipongeza Serikali kwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya madini, yaende kwenye mfuko maalum wa utafiti ambapo kwa kuanzia Wizara ya Madini imetengwa shilingi bilioni 17 za utafiti wa madini.
