Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dkt. Richard Mayungi akifungua mkutano huo kwa niaba ya Naibu Waziri jijini Arusha leo

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere akizungumza kwenye mkutano huo jijini Arusha

……….
Na Happy Lazaro, Arusha
NCHI za Afrika zimetakiwa kuimarisha ushirikiano katika ukaguzi wa mazingira ili kuhakikisha rasilimali za asili zinasimamiwa kwa ufanisi, huku fedha za umma zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya uhifadhi zikitumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Wito huo umetolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, wakati wa Mkutano Mkuu wa 12 wa Mwaka 2026 wa Kikundi Kazi cha Ukaguzi wa Mazingira cha AFROSAI-WGE, unaofanyika jijini Arusha na kushirikisha nchi 32.
Kichere amesema changamoto za mazingira haziheshimu mipaka ya nchi, hivyo ni muhimu kwa taasisi za ukaguzi barani Afrika kushirikiana katika kubaini matatizo, kubadilishana taarifa na kutafuta suluhisho la pamoja kwa changamoto zinazohusu rasilimali zinazotumiwa na mataifa mbalimbali.
Amebainisha kuwa Ziwa Victoria na mfumo wa Mto Nile ni mifano ya rasilimali zinazohitaji usimamizi wa pamoja, kwa kuwa hatua zinazochukuliwa na nchi moja zinaweza kuwa na athari kwa wananchi wa nchi nyingine zinazotegemea vyanzo hivyo.
Amesema taasisi za ukaguzi zinapaswa kuhakikisha serikali zinatimiza ahadi zake za kulinda mazingira, zinatenga fedha katika mipango na bajeti zake na zinatumia rasilimali hizo kwa uwazi ili kufanikisha malengo ya uhifadhi.
Kwa mujibu wa Kichere, ripoti za ukaguzi zinapaswa kuzaa matokeo yanayoonekana katika jamii, yakiwamo ulinzi wa vyanzo vya maji, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuboresha usimamizi wa rasilimali za asili.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dkt. Richard Mayungi, amesema ukaguzi wa mazingira una nafasi muhimu katika kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanaendana na juhudi za kulinda rasilimali zinazochangia maendeleo ya wananchi.
Dkt. Mayungi amesema Afrika ina rasilimali nyingi zikiwamo misitu, madini, wanyamapori na maji, ambazo ni muhimu kwa ustawi wa uchumi na maisha ya watu, hivyo zinahitaji kusimamiwa kwa kuzingatia uwajibikaji na maendeleo endelevu.
Amesema ulinzi wa rasilimali hizo unahitaji mifumo imara ya usimamizi, ushahidi unaotokana na ukaguzi na ushirikiano wa wadau ili kuhakikisha maamuzi yanayofanywa kuhusu mazingira hayaleti madhara kwa vizazi vijavyo.
Ameeleza kuwa Tanzania inatambua umuhimu wa kuhifadhi mazingira katika utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo, ikiwamo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, inayolenga kuimarisha maendeleo ya nchi kwa kuzingatia masuala muhimu ya kitaifa.
Mkutano huo unajadili namna ya kutumia ukaguzi wa mazingira kuimarisha uchumi wa kijani, usalama wa maji na udhibiti wa uchafuzi, huku ukilenga kuongeza uwajibikaji wa taasisi zinazohusika na usimamizi wa rasilimali za asili barani Afrika.
