Na Meleka Kulwa– Fullshangwe Blog, Dodoma
MAMLAKA Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imesema eneo la Makutupora ni chanzo kikuu cha maji kinachoiwezesha kuzalisha sehemu kubwa ya maji yanayotumika jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 26, 2026 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, amesema kwa sasa mahitaji ya maji jijini humo ni lita milioni 159.9 kwa siku, wakati uwezo wa uzalishaji ukiwa lita milioni 91 kwa siku.
Amesema kati ya uzalishaji huo, chanzo cha Makutupora kinazalisha lita milioni 61.5 kwa siku, huku kiasi kingine kikizalishwa kupitia vyanzo vidogo mbalimbali ikiwemo nzuguni, iyumbu, Nala, Ihumwa, nkuhungu, Miganga, Mkonze, na Makulu.
Aidha, amebainisha kuwa DUWASA inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa vyanzo vya maji, ambapo kwa sasa ina visima 72 vinavyofanya kazi katika maeneo mbalimbali, huku visima 17 vilivyopo Makutupora vikitoa sehemu kubwa ya maji yanayozalishwa.
Pia ameongeza kuwa mamlaka hiyo imeandaa mpango wa miaka mitano wa kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 91 hadi lita milioni 121 kwa siku, ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya maji jijini Dodoma.

