NA FAUZIA MUSSA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Anna Athanas Paul, ametoa wito kwa wananchi na wadau wa mazingira kuimarisha juhudi za kuifanya Zanzibar kuwa ya kijani, akisisitiza kuwa maendeleo ya kiuchumi yanapaswa kwenda sambamba na uhifadhi wa mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema hayo wakati akifungua Jukwaa la Pili la Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar na Mkutano Kivuli wa Mabadiliko ya Tabianchi, lililofanyika katika Chuo cha Utalii Maruhubi, Unguja, kwa ushirikiano na Green Samia Foundation.

Anna alisema athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kuwa changamoto inayohitaji hatua za pamoja, ikiwemo kulinda misitu, kupanda miti na kuimarisha uhifadhi wa maeneo ya pwani ili kupunguza athari zinazotokana na uharibifu wa mazingira na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari.

Alieleza kuwa ukataji wa miti ovyo na shughuli nyingine zinazoharibu mazingira vinaongeza hatari kwa mifumo ya ikolojia na maisha ya wananchi, hivyo ni muhimu jamii kubadili mwenendo na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi.

Alisisitiza kuwa jukumu la kuifanya Zanzibar kuwa ya kijani halipaswi kuachwa kwa serikali pekee, bali linahitaji ushiriki wa wananchi, taasisi za umma, sekta binafsi na asasi za kiraia katika kupanda miti na kutunza mazingira katika maeneo yao.

Aidha, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutekeleza mipango ya uhifadhi na kuimarisha hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Mrajisi wa Asasi za Kiraia Zanzibar, Ahmed Khalid Abdulla, alisema taasisi zinazojihusisha na uhifadhi wa mazingira zina wajibu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kupanda na kutunza mikoko, ambayo ina mchango mkubwa katika kulinda maeneo ya pwani.

Alisema ushirikiano baina ya taasisi hizo na jamii ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira ya bahari, ikiwemo uchafuzi unaotokana na kumwagika kwa mafuta machafu.

Aliongeza kuwa ni muhimu hoteli na taasisi nyingine zinazofanya shughuli zake katika maeneo ya pwani kuimarisha usimamizi wa mazingira na kuhakikisha shughuli zao haziendelezi uchafuzi wa bahari, ambayo ni rasilimali muhimu kwa uchumi na ustawi wa Zanzibar.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiko la Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar (ZACCA), Mahfoudh Haji, alisema jukwaa hilo limewakutanisha wawakilishi wa serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na wanaharakati wa mazingira kwa lengo la kujadili changamoto zinazokabili sekta hiyo na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana nazo.

Mahfoudh alisema matumizi ya nishati safi yanapaswa kupewa kipaumbele katika juhudi za kulinda mazingira, akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa na kupunguza athari za kiafya zinazohusishwa na matumizi ya nishati hizo, hasa kwa wanawake wanaotumia muda mwingi kupika.

Mapema alisema shughuli za jukwaa hilo zitahitimishwa Oktoba 26, mwaka huu, kwa hafla ya tuzo za vinara wa mazingira itakayofanyika Palm Hall, Mombasa, Wilaya ya Magharibi B, Unguja.

Katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.