Naibu Katibu Mkuu Dkt. Kedmon Mapana akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Joel Nanauka kwenye Hafla ya Uvunaji wa Samaki wa Vizimba waliofugwa na kikundi cha Kitwima Youth Group.
…………
Na Hellen Mtereko,
Mwanza
Vijana nchini wametakiwa kuendelea kuchangamkia fursa ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba hatua itakayosaidia kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili Oktoba 25, 2026 na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Kedmon Mapana kwaniaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe.Joel Nanauka,
katika Hafla ya Uvunaji wa Samaki wa Vizimba waliofugwa na kikundi cha Kitwima Youth Group baada ya kuwezeshwa kupitia program ya bilioni 200.
Dkt. Mapana amewapongeza vijana hao kwa usimamizi mzuri wa shughuli zao hadi kufikia hatua ya kuvuna samaki.
Aidha, amesema vijana wanapaswa kujisajili kwenye mfumo wa vijana YES (Youth Empowerment System) ili waweze kutambulika na Serikali kupitia Ofisi ya Maendeleo ya vijana iweze kufahamu vipaumbele vyao.
Kwaupande wake Katibu wa Kikundi cha Kitwima Bung’e Nawe Kwaangw, amesema walipewa kiasi cha shilingi milioni 106,963,500 kwaajili ya kutekeleza mradi huo.
Amesema Kikundi hicho kilichopo katika Mwalo wa Luchelele jijini Mwanza kitavuna tani 15 za samaki wenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 127.
“Mafanikio hayo ni hatua kubwa tangu kilipoanza shughuli za ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba”
Naye Kaimu Mkurugenzi wa CRDB Bank Foundation, Fadhili Bushagama, amesema mafanikio ya vijana hao katika kuvuna na kuuza samaki yanaweza kuwa chachu kwa vijana wengine ambao bado wana wasiwasi wa kuthubutu kufanya shughuli za ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.
Bushagama amesisitiza umuhimu wa vijana kuwa waaminifu katika matumizi ya fedha za mikopo na kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati kwani kwakufanya hivyo ni kuendelea kutoa fursa za kifedha kwa vijana wengine.
Nao badhi ya wananchi wameeleza namna mradi huo unavyowanufaisha hususani katika kujipatia kitoweo na kipato cha kukidhi maisha yao.

