NA FAUZIA MUSSA
Zaidi ya wadau 200 wa mazingira wanatarajiwa kukutana Zanzibar kujadili namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha uchumi wa buluu na kubadili taka kuwa fursa za kiuchumi kupitia Jukwaa la Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar na Mkutano Kivuli wa Mabadiliko ya Tabianchi (ZANCCC).
Jukwaa hilo lililoandaliwa na Jumuiko la Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar (ZACCA), linatarajiwa kufunguliwa Oktoba 24 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Anna Athanas Paul, katika Chuo cha Utalii Maruhubi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa ZACCA, Mahfoudh Haji, alisema jukwaa hilo litawakutanisha wawakilishi wa serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na wanaharakati wa mazingira kwa lengo la kujadili changamoto zinazokabili sekta hiyo na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana nazo.
Alisema washiriki kutoka Tanzania na nchi nyingine, zikiwemo Ujerumani, Ethiopia na Kenya, watabadilishana uzoefu kuhusu uhifadhi wa mazingira, uchumi wa buluu na maendeleo endelevu, huku wakitafuta njia za kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa Haji, shughuli za jukwaa hilo zitajumuisha maonesho ya kazi za taasisi zinazojihusisha na mazingira pamoja na vipindi 12 vya majadiliano vitakavyowakutanisha wataalamu kutoka serikalini, wizara na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Alisema mada zitakazojadiliwa ni pamoja na kuendeleza uchumi wa buluu kwa kuzingatia uhifadhi wa rasilimali za bahari, matumizi ya nishati safi na ubunifu wa kuzalisha bidhaa zenye thamani kutokana na taka, ikiwemo mbolea, hatua zinazoweza kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuongeza fursa za ajira na kipato.
Alisisitiza kuwa uchumi wa buluu ni eneo muhimu kwa Zanzibar kutokana na utegemezi wa wananchi katika rasilimali za bahari, hivyo ni muhimu kuhakikisha shughuli za kiuchumi zinaendelezwa kwa njia endelevu bila kuathiri mazingira na rasilimali hizo kwa vizazi vijavyo.
Aliongeza kuwa jukwaa hilo lina vipengele vitatu vikuu ambavyo ni maonesho ya shughuli za wadau wa mazingira, majadiliano ya kitaalamu na utoaji wa tuzo kwa vinara wa mazingira Zanzibar, kwa lengo la kutambua mchango wao katika uhifadhi na kuhamasisha jamii kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Haji alisema kilele cha shughuli hizo kitakuwa Oktoba 26, mwaka huu, kupitia usiku wa tuzo za vinara wa mazingira utakaofanyika Palm Hall, Mombasa, Wilaya ya Magharibi B, Unguja ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Mjini, Mohammed Ibrahim Hassanali (Razalee), aliipongeza ZACCA na wadau wengine kwa kuunga mkono juhudi za serikali za kuimarisha usafi wa miji na kudhibiti taka.
Alisema jukwaa hilo litatoa fursa kwa taasisi za serikali, ikiwemo manispaa, kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu bora za usimamizi wa taka na namna ya kuzigeuza kuwa rasilimali zinazoweza kuleta manufaa ya kiuchumi kwa wananchi.
Razalee alieleza kuwa Manispaa ya Mjini inaendelea kuweka mikakati ya kuimarisha usafi wa mazingira kwa kushirikiana na vikosi vya Idara Maalumu za SMZ, sambamba na juhudi za kutafuta mwekezaji mwenye uwezo wa kukusanya, kusafirisha na kuchakata taka ili kupunguza changamoto ya uchafu katika maeneo ya manispaa hiyo.
Alisema uwekezaji katika uchakataji wa taka unaweza kuongeza uzalishaji wa mbolea na bidhaa nyingine, kufungua fursa mpya za kiuchumi na kuwawezesha wananchi kujiongezea kipato, huku ukichangia kuboresha mazingira ya mijini.
