Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam 

SHIRIKA la Nishati ya Nyuklia la Urusi (Rosatom) limeahidi kushirikiana na Tanzania na nchi nyingine za Afrika kuwaendeleza wanawake katika teknolojia ya nyuklia kupitia mafunzo ya kitaalamu, programu za ulezi na ujenzi wa uwezo ili kuongeza ushiriki wao katika sayansi, uhandisi na ubunifu.

Ahadi hiyo imetolewa katika Jukwaa la Wanawake wa Afrika na Urusi katika Sekta ya Nyuklia la mwaka 2026 lililofanyika Dar es Salaam, likiwakutanisha wataalamu kutoka nchi nane kujadili namna teknolojia ya nyuklia inavyoweza kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi barani Afrika.

Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake ya Rosatom na mjumbe wa Baraza la Jukwaa la Wanawake katika Elimu, Aleksandra Ryabykh, amesema shirika hilo lipo tayari kushirikishana uzoefu na washirika wa Afrika ili kuwaandaa wanawake kushiriki katika sekta za teknolojia za kisasa.

Amesema wanawake wanachangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za Rosatom, ambako wanaunda asilimia 33 ya wafanyakazi, kiwango kinachozidi wastani wa dunia kwa asilimia 10, kwa mujibu wa takwimu zilizotajwa kutoka Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA).

Ameeleza kuwa wanawake nchini Urusi wanashiriki katika maeneo mbalimbali ya sekta ya nyuklia, yakiwamo utafiti wa kisayansi, uhandisi, usanifu wa mitambo ya nyuklia na uendeshaji wa meli zinazotumia nishati hiyo.

Ryabykh amesema kupitia ushirikiano huo, wanawake wa Afrika watanufaika na programu za mafunzo na ulezi wa kitaalamu zitakazowawezesha kupata ujuzi unaohitajika katika sekta ya teknolojia ya hali ya juu na kujiandaa kwa nafasi za uongozi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) na Rais wa Mtandao wa Wanawake katika Sekta ya Nyuklia Tanzania (WiN Tanzania), Profesa Najat Mohammed, amesema maendeleo ya sekta hiyo yanahitaji uwekezaji katika miundombinu pamoja na wataalamu wenye ujuzi wa kutosha.

Amesema Tanzania inaendelea kuchunguza uwezekano wa kutumia nishati ya nyuklia huku ikipanua matumizi ya tiba ya nyuklia, teknolojia ya mionzi na utafiti wa kisayansi, hali inayoongeza mahitaji ya wahandisi, wanafizikia na wataalamu wa usalama wa mionzi.

Profesa Mohammed amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanawake wanapata nafasi katika hatua zote za maendeleo ya sekta hiyo, kuanzia elimu ya kiufundi, ajira katika taasisi za kisayansi na viwanda hadi kushiriki katika michakato ya kufanya maamuzi.

Amesema Mtandao wa Wanawake katika Sekta ya Nyuklia Tanzania, ulioanzishwa mwaka 2025 kwa msaada wa TAEC, umeongeza wanachama kutoka takribani 70 wakati wa uzinduzi hadi kufikia 160, hatua inayodhihirisha kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake katika fani hiyo.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Sayansi na Teknolojia katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Harun Makandi, amesema Afrika inapaswa kuachana na dhana inayohusisha teknolojia ya nyuklia na silaha za kivita pekee na kuitumia kutatua changamoto za afya, maji safi, nishati na maendeleo ya kiuchumi.

Amesema teknolojia hiyo ina fursa kubwa za kuleta suluhisho la changamoto zinazolikabili bara hilo, hivyo wanasayansi, watunga sera, wahandisi na washirika wa maendeleo wanapaswa kushirikiana kubadilishana maarifa na kuhakikisha yanatumika kutatua matatizo halisi ya jamii.

Kwa upande wake, Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Andrey Avetisyan, amesema kuimarisha ushirikiano kati ya Urusi na nchi za Afrika ni muhimu katika kukuza sayansi na teknolojia ya nyuklia, akieleza kuwa kubadilishana uzoefu kunaweza kusaidia kupata suluhisho katika sekta za afya, kilimo na maeneo mengine ya maendeleo.

Naye Rais wa Mtandao wa Wanawake katika Sekta ya Nyuklia Uganda na mtaalamu wa Baraza la Nguvu za Atomiki nchini humo, Ruth Asaba, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza kwa wasichana wadogo ili kuwaandaa kuwa wahandisi na wanasayansi wa nyuklia wa kizazi kijacho.

Jukwaa hilo lililokuwa na kaulimbiu ya “Mazungumzo ya Mabara: Nishati ya Nyuklia kwa Mustakabali wa Baadaye” lilishirikisha Tanzania, Urusi, Misri, Uganda, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia na Afrika Kusini, likilenga kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu na kuongeza mchango wa wanawake katika maendeleo ya teknolojia ya nyuklia.