NAMTUMBO

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, ameiagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuangalia namna ya kuwawezesha wananchi kupata mafunzo na mitaji kwa ajili ya kutengeneza na kusambaza majiko banifu, hatua inayolenga kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Dkt. Homera ametoa agizo hilo leo, Oktoba 24, 2026, wakati wa kushiriki Site Trust Nishati Safi Marathon 2026 iliyofanyika Wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma.

Amesema REA inapaswa kuangalia namna ya kuchagua wananchi watatu kutoka kila wilaya na kuwapatia mafunzo ya kutengeneza majiko banifu kwa kutumia teknolojia rahisi na malighafi zinazopatikana nchini, kisha kuwaunganisha na fursa za mitaji kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, kwa kuzingatia vigezo na taratibu zilizowekwa.

Ameeleza kuwa hatua hiyo itawawezesha wananchi kuanzisha shughuli za uzalishaji na usambazaji wa majiko banifu, kujiajiri na kuongeza upatikanaji wa teknolojia hiyo kwa gharama nafuu, hususan katika maeneo ya vijijini.

“Kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 si kazi ndogo. Ni lazima tufanye jitihada za makusudi za kushirikisha na kuwawezesha wananchi ili wawe sehemu ya kufanikisha lengo hilo,” amesisitiza Dkt. Homera.

Mpango huo unalenga kuunga mkono utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024- 2034, kwa kuongeza ushiriki wa jamii katika uzalishaji na usambazaji wa teknolojia za nishati safi ya kupikia, kulinda afya za wananchi na kuhifadhi mazingira.