Meneja wa Mradi huo,Injinia Dk. Salha Kassim akizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto hiyo iliyojitokeza katika mradi huo jijini Arusha

Na Happy Lazaro, Arusha
.Kampuni ya China Railway Construction Engineering Group (CRCEG), inayotekeleza mradi wa ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mount Kilimanjaro (MKICC) jijini Arusha, imesema changamoto ya kuchelewa kwa mishahara iliyosababisha wafanyakazi kusimamisha kazi kwa muda imetatuliwa, huku shughuli za ujenzi zikiendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto hiyo,Meneja wa Usimamizi wa Hatari katika mradi wa MKICC kutoka kampuni ya CRCEG,Dennis Bennito amesema kuwa ,kampuni hiyo imefafanua kuwa kuchelewa kwa malipo hayo kulitokana na changamoto ya kiufundi katika mifumo ya miamala kati ya kampuni na taasisi za kifedha zilizoshiriki katika mchakato wa malipo.
“Changamoto hiyo ilisababisha mishahara iliyotarajiwa kuingia kwenye akaunti za wafanyakazi Oktoba 20, mwaka huu, kutolipwa kwa wakati.”amesema Bennito.
Amesema kuwa, changamoto hiyo haikusababishwa na kusitishwa kwa wajibu wake wa kulipa mishahara, bali ilihusiana na mifumo ya miamala ya kifedha, na kwamba baada ya kutatuliwa, wafanyakazi wameanza kupokea stahiki zao huku ujenzi ukiendelea.
“Kampuni yetu inathamini mchango wa wafanyakazi, hususani vijana wa Kitanzania wanaoshiriki katika utekelezaji wa mradi huo, na imeahidi kuendelea kuzingatia sheria za kazi za Tanzania pamoja na taratibu zilizowekwa katika kuhakikisha wafanyakazi wanalipwa stahiki zao kwa mujibu wa sheria.”amesema .
Amesema tukio hilo ni la kwanza kutokea katika kipindi cha utekelezaji wa mradi huo, huku ikieleza kuwa inaimarisha uratibu wa mifumo ya malipo ili kupunguza uwezekano wa changamoto kama hiyo kujirudia na kuhakikisha shughuli za ujenzi zinaendelea kwa ufanisi.
Bennito amefafanua kuwa, kampuni inatambua umuhimu wa ushirikiano kati ya wafanyakazi, Serikali na wadau wengine katika kukamilisha mradi huo wa kimkakati, unaolenga kuimarisha nafasi ya Arusha katika sekta ya mikutano ya kimataifa na utalii wa biashara.
“CRCEG imeomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kutokana na tukio hilo na kutoa shukrani kwa wafanyakazi, Serikali kupitia taasisi husika ikiwamo PSSSF, uongozi wa Mkoa wa Arusha na wadau wengine kwa ushirikiano wao katika kushughulikia changamoto hiyo.”amesema Bennito.
Mradi wa MKICC ni sehemu ya juhudi za kuimarisha miundombinu ya mikutano ya kimataifa nchini na kuongeza fursa za utalii wa mikutano, maonesho na biashara, sekta zinazoweza kuchangia shughuli za kiuchumi na ajira kwa Watanzania.
Kwa upande wake Meneja wa Mradi huo,Injinia Dk. Salha Kassim,amesema wafanyakazi hao waligoma kufanya kazi asubuhi kutokana na changamoto ya malipo, hali iliyoufanya uongozi wa mradi kuingilia kati ili kubaini chanzo cha tatizo na kutafuta suluhisho.
Amesema baada ya kupata taarifa za mgomo huo, uongozi uliwaita wafanyakazi hao na kuwasikiliza ili kuelewa malalamiko yao, akibainisha kuwa changamoto hiyo ilihusu malipo wanayopaswa kupata kutoka kwa mwajiri wao ambaye ni mkandarasi, na si madai dhidi ya serikali.
Dk. Kassim amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati ya taifa na kwa sasa umefikia hatua ya utekelezaji wa takribani asilimia 35 hadi 39, huku ukitekelezwa na PSSSF kwa kushirikiana na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Dkt. Salha amesema katika utekelezaji wa mradi huo, kuna pande tatu muhimu ambazo ni mwajiri wa mradi, mshauri elekezi na mkandarasi, kila upande ukiwa na majukumu yake katika kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa viwango na kwa wakati uliopangwa.
Amefafanua kuwa wafanyakazi waliogoma ni wale wanaotekeleza kazi za moja kwa moja eneo la ujenzi, wakiwemo wanaofunga nondo na kumwaga zege, ambao ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa mradi huo.
“Wafanyakazi hao ni kati ya 700 na 800 wanaofika katika eneo la mradi kufanya kazi, lakini changamoto iliyojitokeza ni kutokuwa na mfumo mzuri wa uongozi unaowawezesha kuwasilisha malalamiko yao kwa utaratibu unaofaa.”amesema Dkt.Salha .
Amesema hatua iliyochukuliwa ni kuwataka wafanyakazi hao kuchagua viongozi katika makundi yao ya kazi, pamoja na kumchagua kiongozi atakayewawakilisha kwa ujumla ili kurahisisha mawasiliano kati yao na uongozi wa mradi.
Akizungumzia upande wa malipo ya mkandarasi, Dk. Salha amesema PSSSF kupitia serikali ilimlipa mkandarasi malipo ya awali kwa ajili ya kuanza kazi, huku malipo mengine yakifanyika kulingana na vyeti vya kazi zilizotekelezwa na kuthibitishwa.
Amesisitiza kuwa,PSSSF haina deni la malipo kwa mkandarasi, hivyo changamoto iliyojitokeza ni baina ya wafanyakazi na mwajiri wao, jambo ambalo uongozi wa mradi umeamua kulifuatilia ili lisijirudie tena.
Dkt. Salha ameeleza kuwa baada ya kikao hicho, uongozi uliendelea kukutana na mwakilishi wa wafanyakazi kujadili changamoto zilizowasilishwa, hatua ambayo inalenga kuimarisha mawasiliano na kuhakikisha shughuli za ujenzi zinaendelea bila usumbufu.
Amesema uongozi wa mradi utaendelea kushirikiana na mkandarasi pamoja na wawakilishi wa wafanyakazi katika kutatua changamoto zilizojitokeza, ili kulinda maslahi ya wafanyakazi na kuhakikisha mradi huo wa kimkakati unaendelea kutekelezwa kwa ufanisi.
