Rais wa Chama cha Wataalamu wa Optometria Tanzania (TOA) Henry Ngogo akizungumza jijini Arusha
Mjumbe wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo,Salma Kilima akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo jijini Arusha
Msajili Baraza la Optometria chini ya Wizara ya Afya, Sebastiano Millanzi akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha
Washiriki wa mkutano huo wakifuatilia mada mbalimbali katika mkutano huo jijini Arusha
( Picha zote na Fullshangwe Blog – Arusha)
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha .Rais wa Chama cha Wataalamu wa Optometria Tanzania (TOA) Henry Ngogo amesisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za afya ya macho nchini kupitia elimu kwa wananchi, ushirikiano wa kitaaluma na mafunzo endelevu kwa wataalamu ili kukabiliana na changamoto za matatizo ya macho.
Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza kwenye mkutano wa Chama cha wataalamu wa Optometria Tanzania (TOA) uliowashirikisha wataalamu hao kutoka mikoa mbalimbali.
Amesema kuwa ,mkutano huo unalenga kujadili changamoto zinazowakabili, kubadilishana uzoefu na kujifunza maendeleo mapya ya teknolojia yanayoweza kuboresha huduma za afya ya macho kwa jamii.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wataalamu kushirikiana katika kutoa huduma bora na kuhamasisha wananchi kupima macho mara kwa mara ili kubaini matatizo mapema na kupata matibabu stahiki.
Naye Mjumbe wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo,Salma Kilima amesema shughuli za utoaji huduma za afya ya macho kwa jamii ni sehemu muhimu ya mkutano wa TOA unaofanyika jijini Arusha.
Salma amesema zoezi hilo limehusisha wataalamu wa optometria pamoja na wataalamu wengine wa afya ya macho, ambao wamewapatia wananchi huduma na kuwaelekeza wagonjwa wanaohitaji matibabu zaidi kwenye vituo vinavyofaa.
“Mafunzo yanayotolewa katika mkutano huo yanawawezesha wataalamu kupata ujuzi kuhusu miongozo na teknolojia mpya, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kuboresha huduma za afya ya macho nchini.”amesema Salma .
Aidha, amewahimiza wataalamu wa optometria ambao bado hawajajiunga na chama chao kufanya hivyo ili kuimarisha ushirikiano, kutetea maslahi ya kitaaluma na kukuza maendeleo ya fani hiyo nchini.
Aidha amewaonya wanaouza miwani holela bila kufanya uchunguzi wa kitaalamu wa macho, kwani vitendo hivyo vinaweza kuhatarisha afya ya wananchi na kusababisha matatizo ya macho kutogundulika mapema.
“Mtu mwenye changamoto ya kuona anapaswa kufika kwa mtaalamu wa macho kwa uchunguzi kabla ya kutumia miwani, ili kubaini chanzo cha tatizo na kupata suluhisho linalofaa badala ya kujitibu mwenyewe.”amesema Salma .
Kwa upande wake Msajili Baraza la Optometria chini ya Wizara ya Afya, Sebastiano Millanzi amesema hadi sasa Baraza limesajili wataalamu 536 na linaendelea kuimarisha mifumo ya usajili na usimamizi ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Amesema wahitimu wapya wanaofaulu mitihani husika husajiliwa awali na kufanya kazi chini ya usimamizi wa wataalamu wenye sifa kwa kipindi cha mwaka mmoja katika vituo vya afya vya umma au binafsi ili kupata uzoefu wa kitaaluma.
“Nawaomba wataalamu kuzingatia maadili na mipaka ya majukumu yao, kwani kutoa huduma nje ya uwezo wa kitaaluma kunaweza kuhatarisha afya ya wagonjwa na nawaomba kushirikiana na madaktari bingwa na wataalamu wengine ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma zinazolingana na mahitaji yao.”amesema Millanzi.
Naye Mtaalamu wa Optometria kutoka Hospitali ya mji Bariadi Eliabu Mbuguma amesema ongezeko la matatizo ya macho duniani linachangiwa na mambo mbalimbali, ikiwemo kuongezeka kwa umri wa kuishi, matumizi ya muda mrefu ya vifaa vya kidijitali na mabadiliko ya maisha mijini.
Amesema matumizi ya muda mrefu ya simu na kompyuta, hasa kwa watoto, yanaweza kuchangia ongezeko la myopia, hali inayosababisha mtu kuona vitu vilivyo mbali kwa ukungu.
Aidha ameshauri watoto kupata muda wa kutosha wa kucheza nje na kusisitiza umuhimu wa kutenga maeneo salama ya michezo, huku akiwataka wananchi kupima macho kwa wataalamu wenye sifa kabla ya kutumia miwani ili kuhakikisha wanapata vipimo sahihi.
