NA FAUZIA MUSSA
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Abdulla Said, ameitaka Taasisi ya Elimu Zanzibar kuhakikisha vitabu vya ziada vinapatikana katika maktaba za serikali na mifumo ya kidijitali ili kuimarisha umahiri wa kusoma, kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi.
Alitoa wito huo wakati wa makabidhiano ya vitabu vilivyoandaliwa na Taasisi ya Elimu Zanzibar kwa kushirikiana na shirika la Room to Read, akisisitiza umuhimu wa kuviweka katika mfumo wa PDF ili wanafunzi waweze kuvisoma kupitia mtandao na vifaa vya kielektroniki.
Alisema vitabu hivyo vinapaswa kuwa na vielelezo na michoro yenye mvuto na kuzingatia mazingira na utamaduni wa Zanzibar ili kuwahamasisha watoto kupenda kusoma na kuishauri Taasisi ya Elimu kuendelea kuboresha maudhui na uhariri wa matoleo yajayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Room to Read nchini Tanzania, Joan Ndaambuyo Minja, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano katika kutekeleza programu za usomaji na maktaba zinazolenga kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.
Alisema shirika hilo linashirikiana na Taasisi ya Elimu Zanzibar kuandaa vitabu vya ziada na nyenzo za walimu, huku vitabu hivyo vikifanyiwa tathmini ili kuhakikisha vinakidhi mahitaji ya wanafunzi.
Naye Mrajisi wa Asasi za Kiraia, Ahmed Abdullah, alisema ushirikiano huo utasaidia kukabiliana na uhaba wa vitabu, kuongeza ujuzi wa walimu na kuboresha ufaulu wa wanafunzi.
Aidha alisisitiza umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa vitabu vinavyozingatia mila, silka, lahaja na mitaala ya Zanzibar.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Misingi na Maandalizi, Fatma Ramadhan Mode, alisema vitabu hivyo vitatumika kwa wanafunzi wa darasa la kwanza katika hatua ya majaribio ili kutathmini mchango wake katika kuimarisha stadi za msingi.
Jumla ya vitabu 3,534 vilikabidhiwa, vikiwemo vitabu 110 vya mwongozo wa mwalimu na vitabu 3,424 vya ziada kwa wanafunzi.

