Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe akizungumza kwenye mkutano huo mkoani Arusha

Mkurugenzi Mkuu wa ECSA,Dokta Ntuli Kapologwe akizungumza kwenye mkutano huo jijini Arusha

…………..
Na Happy Lazaro, Arusha
Serikali imeelekeza umuhimu wa kuwashirikisha vijana katika maamuzi ya mipango na bajeti za afya ili kuhakikisha changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi na kuboresha huduma zinazohusiana na afya ya uzazi, afya ya akili na huduma rafiki kwa vijana nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amesema vijana wanapaswa kushirikishwa katika hatua za kupanga na kuamua vipaumbele vya afya, huku maoni yao yakigeuzwa kuwa mikakati inayoweza kutekelezwa na kupimwa matokeo yake.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa mazungumzo ya vijana ulioandaliwa na Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA Health Community), Prof. Shemdoe amesema TAMISEMI ina nafasi muhimu katika kutatua changamoto hizo kupitia zahanati, vituo vya afya na hospitali zinazosimamiwa na halmashauri.
Amesisitiza kuwa mapendekezo ya vijana yanapaswa kuingizwa katika mipango na bajeti za Serikali, yakiambatana na muda maalumu wa utekelezaji na vigezo vya kupima mafanikio, ili kuhakikisha mijadala inayofanyika inazaa matokeo yanayoonekana katika jamii.
Aidha, Prof. Shemdoe ametoa wito wa kuzingatia mahitaji ya vijana wa kiume na wa kike katika huduma za afya ya uzazi, akieleza kuwa maandalizi ya familia bora yanahitaji jinsia zote kushirikishwa kwa usawa na kupewa huduma zinazokidhi mahitaji yao halisi.
Mkurugenzi Mkuu wa ECSA,Dokta Ntuli Kapologwe amewataka vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar kushiriki kikamilifu katika juhudi za kupunguza vifo vya mama na watoto, kuimarisha upatikanaji wa chanjo kwa watoto wote na kuhakikisha wanawake wajawazito wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Aidha mkutano huo wa vijana umewajumuisha washiriki takribani 200 kutoka maeneo mbalimbali nchini, kwa lengo la kujadili afya ya uzazi kwa vijana, afya ya akili na namna ya kushirikiana kutekeleza malengo ya *Zero Sifuri Tatu* yanayolenga kuimarisha afya ya mama na mtoto.
Dkt.Kapologwe amesema kuwa, mkutano huo ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha vijana kushiriki katika utekelezaji wa afua za afya ya uzazi na mtoto, akisisitiza kuwa uwekezaji kwa vijana ni muhimu kutokana na nafasi yao katika jamii.
Amefafanua kuwa,vijana wanapaswa kupewa elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi na afya ya akili, huku wakihamasishwa kushiriki katika kuzuia mimba za utotoni na changamoto nyingine zinazoweza kuhatarisha maisha ya wasichana, wanawake wajawazito na watoto.
“mkutano huo pia unalenga kuimarisha ushirikiano baina ya wizara mbalimbali, akibainisha kuwa masuala ya afya ya mama na mtoto hayawezi kutatuliwa na Wizara ya Afya pekee, bali yanahitaji mchango wa sekta nyingine zikiwemo michezo, habari, sanaa na utamaduni.”amesema Dkt.Kapologwe .
Kwa upande wake, Mwakilishi wa vijana vinara wa ECSA -HC Network,Dkt.Kuduishe Kisowile amesema vijana watatumia mkutano huo kujadili namna wanavyoweza kuchangia utekelezaji wa malengo ya *Zero Sifuri Tatu*, ikiwemo kuzuia vifo vya mama na mtoto, kuhakikisha watoto wanapata chanjo na kupunguza wanawake wanaojifungulia nyumbani.
Amesema mimba za utotoni ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji kushughulikiwa kwa ushirikiano, hivyo vijana wanapaswa kushirikishwa katika kutoa elimu na kuhamasisha wenzao kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya ya uzazi.
Ameongeza kuwa matumizi ya michezo, sanaa na tamaduni yanaweza kuwa njia muhimu ya kufikisha ujumbe wa afya kwa vijana wengi zaidi, huku akisisitiza umuhimu wa wizara na taasisi mbalimbali kushirikiana katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili vijana.
Dkt.Kisowile ameeleza kuwa washiriki wa mkutano huo wanatoka katika maeneo na taasisi mbalimbali zinazoongozwa na vijana, hivyo wanatarajia kutumia nafasi hiyo kujenga mtandao utakaowezesha maazimio yatakayofikiwa kuwafikia vijana wengi zaidi nchini.
Amesema baada ya mkutano huo, vijana watasambaza ujumbe na maazimio kupitia majadiliano katika maeneo wanayoishi, mitandao ya kijamii na majukwaa ya mtandaoni ikiwemo *webinar*, ili kuwafikia wale ambao hawakupata nafasi ya kushiriki moja kwa moja.
Mkutano huo unatarajiwa kuwa jukwaa la kubadilishana mawazo na uzoefu kuhusu afya ya uzazi, afya ya akili na nafasi ya vijana katika kuunga mkono juhudi za kupunguza vifo vya mama na watoto, pamoja na kuimarisha huduma za afya kwa makundi hayo.
Mkutano huo, umeandaliwa na Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC) kwa kushirikiana na wadau wengine wa sekta ya afya, umebeba kaulimbiu “Kutoka Ahadi Hadi Vitendo, Vijana Wakiwa Vinara wa Mabadiliko.
