Dodoma

Askofu Mkuu wa Kanisa la Spiritual Pentecostal Church of Tanzania (SPCT), Dkt. Musa Samsoni Mlawi, ameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya barabara na kupanga mji wa Chamwino kisasa ili uendane na hadhi yake kama eneo lilipo Ikulu ya Tanzania.

Akizungumza Chamwino,  Mlawi, ambaye pia ni Rais ( r ) wa Tanzania Pastors Association (TPA), amesema eneo hilo linahitaji kuendelezwa kwa kuzingatia umuhimu wake wa kitaifa, ikiwemo kuboresha barabara na kupanga vizuri maeneo ya makazi, biashara na kata zinazolizunguka.

Amesema upangaji mzuri wa mji huo utasaidia kuendana na mahitaji ya sasa ya maendeleo na kuhakikisha Chamwino inakua kwa utaratibu unaozingatia mahitaji ya wananchi na shughuli za Serikali.

“Ni vizuri kuikumbuka Chamwino ili iweze kuendana na teknolojia iliyopo, ikue na kuendelea kukua, pamoja na kuboresha mji huo kama sehemu yenye umuhimu mkubwa katika shughuli za Serikali,” amesema.

Amesisitiza kuwa maendeleo ya Chamwino yanapaswa kuhusisha zaidi ya ujenzi wa barabara, kwa kuangalia pia mpangilio wa mji na maeneo ya jirani ili kuboresha mazingira ya makazi na biashara.

Katika hatua nyingine, Mlawi amesema anaendelea kuliombea taifa, Serikali na Kanisa la Mungu duniani, akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, mshikamano, upendo na utulivu miongoni mwa Watanzania.

Amesema anaendelea kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na viongozi wengine wa Serikali, ili waongozwe kwa hekima na busara katika kutekeleza majukumu yao na kusimamia utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumzia historia yake ya kushiriki katika shughuli za kisiasa, Mlawi amesema anamfahamu Makamu wa Rais kutokana na kipindi walichoshiriki pamoja katika shughuli za kisiasa wakati Makamu wa Rais alipokuwa akitafuta nafasi ya ubunge.

Amesema ataendelea kuzungumzia masuala mbalimbali ya maendeleo yanayowagusa wananchi, yakiwemo changamoto zinazowakabili wakulima na makundi mengine ambayo, kwa mtazamo wake, yanahitaji kupewa kipaumbele zaidi katika mipango ya maendeleo.