Na Silivia Amandius, Kagera

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetoa mafunzo kwa maafisa na watoa huduma kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA), yakilenga kuimarisha huduma kwa wateja, kuongeza weledi kwa watumishi na kupunguza malalamiko yanayojitokeza katika utoaji wa huduma za maji mkoani Kagera.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, Bw. Nyirabu Musira, amesisitiza umuhimu wa watumishi kuzingatia taratibu za utoaji wa huduma, kutumia lugha yenye staha, kuwasikiliza wateja kwa makini na kushughulikia changamoto zao kwa wakati. Amesema hatua hizo ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa huduma na kuridhisha wananchi wanaotegemea huduma za maji.

Kwa upande wake, Afisa Huduma kwa Wateja kutoka EWURA, Bi. Jessica Sewando, amewahimiza wateja kusoma na kuelewa Sheria ya Maji ili kufahamu haki na wajibu wao. Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi kutoa taarifa mapema wanapobaini upotevu wa maji au uharibifu wa miundombinu ya maji, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza hasara, kulinda miundombinu na kuboresha upatikanaji wa huduma za maji.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa BUWASA, Bi. Devotha Koy, ameiomba EWURA kuendelea kutoa mafunzo hayo mara kwa mara ili kuongeza ujuzi na maarifa kwa watumishi. Pia, amewakumbusha wateja kulipa bili za maji kwa wakati ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza katika upatikanaji wa huduma. Wakati huohuo, Kaimu Mkurugenzi wa BUWASA, Bi. Julieth Shangali, ameishukuru EWURA kwa mafunzo hayo na kueleza kuwa yatasaidia kuboresha mahusiano kati ya watumishi na wateja.

Shangali amesisitiza kuwa BUWASA itazingatia na kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa, ikiwemo kuwahudumia wateja kwa lugha nzuri, kuwasikiliza na kutatua changamoto zao kwa wakati. Ameeleza kuwa utekelezaji wa mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kupunguza malalamiko, kuongeza ufanisi na kujenga imani ya wananchi kwa mamlaka hiyo katika utoaji wa huduma za maji.