Viongozi wa halmashauri nchini wametakiwa kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unawafikia wananchi katika maeneo yao, ili kupunguza mzigo wa gharama za matibabu, hususan kwa wananchi wenye kipato cha chini.
Wito huo umetolewa Oktoba 22, 2026, na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Mhe. Jabir Shekimweri, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mpango wa Bima ya Afya kwa Wote mkoani Dodoma.
Shekimweri amesema mafanikio ya mpango huo hayatapimwa kwa idadi ya mikutano inayofanyika au mabango ya elimu yanayowekwa, bali kwa uwezo wa wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu mpango huo, kujiunga na bima ya afya na kupata huduma za matibabu wanapozihitaji.
Amesisitiza umuhimu wa viongozi wa halmashauri kuhakikisha elimu kuhusu Bima ya Afya kwa Wote inawafikia wananchi katika maeneo yote, ili kuongeza uelewa na kuhamasisha ushiriki wao katika mpango huo.
Kwa upande wake, Meneja wa Mfuko wa Bima ya Afya Mkoa wa Dodoma, Irene Kataraihya, amesema mpango huo unalenga kuondoa vikwazo vya gharama za matibabu kwa kuwawezesha wananchi kupata huduma za afya katika ngazi mbalimbali za vituo vya kutolea huduma.
Amesema huduma hizo zitapatikana kuanzia zahanati na vituo vya afya hadi hospitali za wilaya na mkoa, kwa kuzingatia utaratibu wa rufaa, hatua inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Aidha, Kataraihya ameeleza kuwa kaya zisizo na uwezo wa kumudu gharama za kujiunga na bima zitasaidiwa na Serikali, huku wananchi wenye uwezo wakihimizwa kujiunga kupitia utaratibu wa Bima ya Afya kwa Wote au kupitia vikundi vyao.
Mpango huo unatarajiwa kuwa na mchango muhimu katika kupunguza changamoto za gharama za matibabu kwa wananchi na kusaidia familia kupata huduma za afya bila kukabiliwa na mzigo mkubwa wa kifedha.
