Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeungana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika juhudi za kuimarisha uongozi, mshikamano na mtangamano wa kikanda kupitia Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika kwa njia ya mtandao, Oktoba 21, 2026.

Kwenye ngazi ya Mawaziri, Tanzania iliwakilishwa katika mkutano huo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel William Shelukindo, ambapo viongozi walijadili masuala muhimu yanayohusu uongozi na uendeshaji wa taasisi za jumuiya hiyo.

Mkutano huo uliitishwa kwa madhumuni ya kuridhia uteuzi wa Naibu Katibu Mtendaji wa SADC anayeshughulikia Mtangamano wa Kikanda, pamoja na kumchagua Mwenyekiti ajaye wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC.

Hatua hizo ni sehemu ya jitihada za jumuiya hiyo za kuimarisha mifumo ya uongozi na ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama, hususan katika masuala ya amani na usalama, ili kuweka mazingira bora ya kuendeleza mtangamano na maendeleo endelevu katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.