Na Mwandishi wetu

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imezindua rasmi Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima kwa mwaka 2025, inayoonesha ukuaji wa sekta ya bima nchini kupitia ongezeko la mtaji, uwekezaji, ada za bima, ajira na idadi ya wananchi wanaonufaika na huduma hizo. Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika Oktoba 16, 2026, jijini Dodoma, Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware, amesema sekta hiyo imeendelea kukua na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.Dkt. Saqware amesema kati ya mwaka 2024 na 2025, mtaji halisi wa sekta ya bima umeongezeka kutoka shilingi bilioni 697.4 hadi shilingi trilioni 1.89, huku uwekezaji ukiongezeka kutoka shilingi trilioni 1.41 hadi shilingi trilioni 2.24. Aidha, mali za sekta hiyo zimeongezeka kutoka shilingi trilioni 2.14 hadi shilingi trilioni 4.06, wakati ada za bima zilizoandikishwa zimeongezeka kutoka shilingi trilioni 1.52 hadi shilingi trilioni 2.55 katika kipindi hicho.

Ameeleza kuwa idadi ya wakata bima na wanufaika imeongezeka kutoka watu milioni 25.9 mwaka 2024 hadi milioni 26.8 mwaka 2025, sawa na ongezeko la takribani asilimia 3.5. Kati ya watu hao, wakata bima ni milioni 8.7 na wanufaika ni milioni 18.1. Vilevile, ajira rasmi katika sekta ndogo ya bima zimeongezeka kutoka 3,000 hadi 6,434 ndani ya miaka mitano, sawa na ongezeko la takribani asilimia 114.5.Akizungumzia viashiria vingine vya ukuaji wa sekta hiyo, Dkt. Saqware amesema mchango wa bima katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 1.8 hadi asilimia 2.8 mwaka 2025. Aidha, uandikishaji wa bima za kawaida umeongezeka kwa asilimia 44, bima za afya kwa asilimia 38.6 na bima za maisha kwa asilimia 14, huku bima mtawanyo na bima za Takaful zikionesha ukuaji wa asilimia 0.3. Ameongeza kuwa TIRA inalenga kukamilisha Sera ya Taifa ya Bima, kuboresha sheria na kanuni zinazosimamia sekta hiyo, pamoja na kuendeleza sekta ya bima kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (FSDMP) wa mwaka 2030.