Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Kushoto) akiwa katika picha na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki ya Dunia anayemaliza muda wake, Dkt. Zarau Kibwe, walipokutana na kufanya mazungumzo, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia, jijini Bangkok, Thailand
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (wa tatu kushoto), Waziri wa Fedha-Zanzibar, Mhe. Dkt Juma Malik Akil (wa pili kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (wa tatu kulia), Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Tausi Kida (kulia), Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki hiyo anayemaliza muda wake, Dkt. Zarau Kibwe (wa pili kulia), Mkurugenzi Mbadala wa Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki ya Dunia, Bi. Lonkhululeko Magagula, wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mazungumzo yao, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia, jijini Bangkok, Thailand.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiongoza kikao na ujumbe wa Benki ya Dunia ukiongozwa na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki hiyo anayemaliza muda wake, Dkt. Zarau Kibwe, walipokutana na kufanya mazungumzo kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia, jijini Bangkok, Thailand.
……….,…
Na. Joseph Mahumi, Bangkok, Thailand
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake katika kuimarisha ushirikiano wa maendeleo na Tanzania, hususan katika ufadhili wa miradi ya kimkakati, maendeleo ya rasilimali watu, nishati na miundombinu ya usafirishaji, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya wananchi na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki hiyo anayemaliza muda wake, Dkt. Zarau Kibwe, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia, jijini Bangkok, Thailand.
Mhe. Balozi Omar aliishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake katika maendeleo ya sekta ya nishati, akibainisha kuwa ushirikiano huo umechangia juhudi za kupanua upatikanaji wa umeme na kuimarisha miundombinu ya nishati, sambamba na mpango wa Mission 300 unaolenga kuongeza upatikanaji wa umeme barani Afrika.
“Tanzania imenufaika na ufadhili wa IDA-20 wa karibu dola bilioni sita za Marekani, huku chini ya IDA-21 tukipangiwa dola bilioni 2.54 za Marekani na ahadi za ufadhili zinazozidi dola milioni 760, huku miradi mingine ikiendelea kuandaliwa kwa ajili ya utekelezaji” alisema Mhe. Balozi Omar
Akizungumzia ukubwa wa ushirikiano wa sasa kati ya Tanzania na Benki ya Dunia, Mhe. Balozi Omar amesema kuwa thamani ya miradi 33 inayotekelezwa kupitia ushirikiano huo imefikia zaidi ya dola bilioni 8.8 za Marekani, ambapo miradi 30 ni ya kitaifa na mitatu ni ya kikanda, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu na kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha shughuli za kiuchumi na usafirishaji Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Katika eneo la usafirishaji, Mhe. Balozi Omar alisema Serikali inaendelea kushirikiana na Benki ya Dunia katika kuboresha Ushoroba wa Kati (Central Corridor), kwa kuzingatia umuhimu wa kuunganisha bandari, reli na miundombinu mingine ya usafirishaji ili kurahisisha biashara na kuongeza fursa za uwekezaji.
“Serikali inalenga kuubadilisha Ushoroba wa Kati kutoka njia ya usafirishaji na kuufanya kuwa Ushoroba wa Maendeleo na Ustawi wa Kiuchumi (Economic Prosperity Corridor), kwa kutambua na kuendeleza fursa za uwekezaji, kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo yanayopitiwa na miundombinu hiyo.” alisema Mhe. Balozi Omar.
Aliongeza kuwa Tanzania inathamini mchango wa Dkt. Kibwe katika kufanikisha majukwaa muhimu ya kimataifa yaliyofanyika nchini, yakiwemo Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu Rasilimali Watu (Human Capital Summit) uliofanyika Dar es Salaam mwezi Julai 2023, pamoja na Mkutano wa Mapitio ya Katikati ya Kipindi cha Mfuko wa Maendeleo wa Kimataifa (IDA) uliofanyika Zanzibar mwezi Desemba 2024.
Ameeleza kuwa mikutano hiyo imeipa Tanzania fursa ya kuimarisha nafasi yake katika mijadala ya maendeleo ya Afrika na kimataifa, hususan katika kuboresha rasilimali watu, ambayo ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi na kukabiliana na changamoto za maendeleo barani Afrika.
Mhe. Balozi Omar alieleza matumaini ya Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano na Mkurugenzi mpya atakayechukua nafasi hiyo Bi. Lonkhululeko Magagula, atakayechukua nafasi hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki hiyo anayemaliza muda wake, Dkt. Zarau Kibwe, ameipongeza Tanzania kwa hatua zilizopigwa katika kuimarisha ushirikiano wake na Benki ya Dunia, akibainisha kuwa thamani ya miradi ya maendeleo kati ya pande hizo imeongezeka kutoka takribani dola bilioni nne alipokuwa akianza majukumu yake hadi kufikia kiwango cha sasa.
Alisema mafanikio hayo yanaonesha hatua kubwa iliyofikiwa katika kuimarisha ushirikiano na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku akieleza kuwa akiwa Benki ya Dunia, anajivunia kushuhudia Tanzania ikifikia hadhi ya nchi yenye uchumi wa kipato cha kati.
Dkt. Kibwe alisisitiza umuhimu wa Tanzania kuendelea kutumia fursa za uwekezaji katika miundombinu na maendeleo ya sekta ya madini, akieleza kuwa nchi hiyo ni miongoni mwa nchi 30 zinazozingatiwa katika mpango wa Benki ya Dunia unaolenga kuimarisha maendeleo ya sekta ya madini na rasilimali zake.
“Mpango huu unajumuisha maeneo muhimu matatu ambayo ni kuimarisha utawala na usimamizi wa sekta ya madini, kuendeleza miundombinu inayowezesha uchimbaji na usafirishaji wa madini, pamoja na kuongeza upatikanaji wa mitaji na uwekezaji katika sekta hiyo” alisema Dkt. Kibwe.
Mazungumzo hayo yameonesha dhamira ya Tanzania ya kuendeleza ushirikiano na washirika wake wa maendeleo ili kutumia fursa za ufadhili, uwekezaji na utaalamu katika kutekeleza miradi ya kimkakati na kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha-Zanzibar, Mhe. Dkt Juma Malik Akil, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, na maafisa wengine waandamizi wa Serikali na Benki ya Dunia.

