Na Mwandishi wetu, Mirerani
GLISTEN Pre & Primary School iliyopo mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imejipanga kikamilifu kuendelea kujiimarisha kitaaluma ili kuhakikisha wanafunzi wanaohitimu shuleni hapo wanapiga hatua katika masomo yao.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Denis Costantin akizungumza baada ya wanafunzi 60 kufanya mahafali ya sita ya shule hiyo amesema Glisten imekuwa na ufaulu mzuri kwa ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Mwalimu Denis amesema Glisen yenye wanafunzi 628 inajivunia kuwa mahali bora pa kufunza watoto, kukuza na kuandaa viongozi bora wa kesho ijayo.
Amesema wamekuwa wakiwapa nafasi wanafunzi wa shule hiyo kuonyesha vipaji walivyonavyo ikiwemo michezo, sanaa, uimbaji na shughuli za kijamii.
“Tunaamini kiwa elimu bora siyo kupata alama nzuri pekee bali pia kujenga tabia njema ndiyo sababu tumekuwa tukiwahimiza wanafunzi kuwa na heshima, uaminifu, bidii, uwajibikaji na ushirikiano,” amesema mwalimu Denis.
Meneja wa shule hiyo, Justice Justin Nyari amewatakia kila la heri wahitimu hao watakaoanza safari mpya ya elimu ngazi ya sekondari mwaka 2027.
Justice amewaasa wahitimu kuchangua marafiki bora na wazuri ili waendeleze nidhamu waliyokuwa nayo shuleni hapo, waliposoma kwa heshima na bidii.
Mgeni rasmi wa mahafali hayo, Meneja wa shirika la ugavi wa nishati ya umeme (TANESCO) Wilaya ya Mirerani, mhandisi Mulam Chomola amepongeza walimu wa Glisten kwa namna bora wanavyotoa taaluma.
Mhandisi Chomola amesema shule hiyo inasifika kwa taaluma bora kwa wanafunzi ndiyo sababu wajukuu zake wawili wanasoma katika shule hiyo.
Mmoja kati ya wahitimu wa shule hiyo John Toima Makeseni ambaye lengo lake ni kuwa daktari na amepongeza walimu wake kwa kipindi chote cha miaka saba waliyomfundisha.
Mhitimu mwingine Nathan Innocent Vitalis amesema matarajio yake ya baadaye ni kuendelea kusoma kwa bidii elimu ya sekondari, chuo hadi awe rubani.
Mhitimu mwingine Bless Nelson Ringo ameeleza kuwa atajiendeleza vyema kielimu kwa ngazi zinazofuata ili aweze kuja kuwa daktari.
