Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi.

Katibu Mkuu wa CWT, Mwl. Protas Magesa,

………..

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi, amekitaka Chama cha Walimu Tanzania na Vyama vya wafanyakazi nchini kubuni na kuwekeza katika miradi ya kiuchumi itakayozalisha ajira, badala ya kujikita katika kudai haki za wafanyakazi pekee.

Dkt. Munisi ameyasema hayo leo, Oktoba 16, 2026, Jijini Mbeya, wakati akifungua mafunzo kwa Wenyeviti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), yanayofanyika kwa siku mbili, kuanzia Oktoba 16 hadi 17, 2026, katika Ukumbi wa City Park.

Amesema, Vyama vya wafanyakazi ni muhimu katika kukuza uchumi na shughuli za kijamii, hivyo zinazopaswa kushiriki kikamilifu katika kukuza fursa za ajira nchini, akitolea mfano CWT ambayo imefanikiwa kuajiri watumishi 401.

“Vyama vya wafanyakazi havipaswi kuonekana kama vyombo vya madai pekee; ni taasisi muhimu za kiuchumi na kijamii zinazopaswa kukuza na kuzalisha fursa za ajira nchini.

“CWT imethibitisha hili kwa kuajiri watumishi 401. Rai yangu kwenu na kwa vyama vingine vya wafanyakazi ni kuendelea kubuni miradi ya kiuchumi na kisekta inayozalisha ajira mpya na kuhakikisha taarifa za ajira hizo zinaripotiwa kikamilifu katika mamlaka husika ili takwimu hizo ziingizwe kwenye mchango wa sekta binafsi na asasi katika ukuzaji wa fursa za ajira nchini,” amesema Dkt. Munisi.

Aidha, amesisitiza kuwa ajira zitakazozalishwa na vyama vya wafanyakazi zinapaswa kuwa ajira za staha, zinazozingatia sheria, haki za wafanyakazi na mazingira bora ya kazi.

Kadhalika, ametaka vyama hivyo kuhakikisha vinalipa kodi za Serikali kwa mujibu wa sheria na kuwasilisha michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii, ikiwemo NSSF, pamoja na michango ya bima ya afya kwa wakati.

Pia, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia viwango vya usalama na afya mahali pa kazi vinavyosimamiwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), kuchangia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na kuzingatia muda wa kazi kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini.

Awali, akiwasilisha risala kwa mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa CWT, Mwl. Protas Magesa, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa mafunzo unaoendelea kutekelezwa na chama hicho.

Amesema mafunzo mengine yaliyotolewa mwaka 2026 ni pamoja na mafunzo kwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Taifa, makatibu wa chama wa mikoa na wilaya nchini kote, pamoja na walimu wenye ulemavu katika mikoa ya Dodoma, Iringa na Njombe.

Ameeleza kuwa chama hicho pia kimeshiriki katika vikao vya wadau wa elimu, wakiwemo Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Taasisi ya Elimu Tanzania, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na wadau wengine wa maendeleo ya elimu nchini.