Na Mwandishi Wetu– Dar es Salaam
Wanawake 399 kutoka makundi manane ya kwanza wamehitimu Programu ya Uongozi wa Wanawake inayoendeshwa na Taasisi ya UONGOZI, inayolenga kuwawezesha wanawake kukabiliana na changamoto za uongozi na kuimarisha uwezo wao wa kudumu katika nafasi za maamuzi.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Kadali Singo, ameeleza hayo Oktoba 12, 2026, wakati akiwasilisha mada katika Jukwaa la Uongozi wa Wanawake lililofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Singo amesema programu hiyo inalenga kuwaendeleza wanawake wa Kiafrika walio katika ngazi za kati na za juu za uongozi katika sekta mbalimbali, kwa kuwapatia maarifa na mbinu za kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika safari zao za uongozi.
Amesema programu hiyo ina muda wa miezi sita na inatekelezwa kwa ushirikiano na Shule ya Usimamizi ya Chuo Kikuu cha Yale (Yale School of Management), ikiwa na lengo la kuwaimarisha wanawake katika kufikia na kudumu katika nafasi za juu za uongozi.
Programu hiyo ina vipengele vitatu vikuu ambavyo ni mafunzo ya uongozi, ushauri wa kitaalamu (coaching) pamoja na ushauri elekezi na ufuatiliaji wa maendeleo (mentoring), vinavyolenga kujenga uwezo wa washiriki katika kutekeleza majukumu yao.
Kupitia vipengele hivyo, washiriki wanapata fursa ya kutambua mitindo yao ya kipekee ya uongozi, kuandaa mipango binafsi ya maendeleo na kujenga mitandao ya kitaaluma itakayowasaidia kubadilishana uzoefu na viongozi wengine.
Maelezo yaliyowasilishwa katika jukwaa hilo yanaonesha kuwa programu hiyo imefikia makundi 10, huku kila kundi likiwa na wanawake viongozi 50 kutoka sekta mbalimbali.
Wahitimu 399 wa makundi manane ya kwanza ni sehemu ya juhudi za kuwaendeleza wanawake katika sekta za umma, binafsi na sekta nyingine, kwa kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazoweza kuathiri maendeleo yao ya kiuongozi.
Jukwaa hilo pia limeangazia changamoto zinazoendelea kuwakabili wanawake katika kupata nafasi za uongozi na kudumu katika nafasi hizo, licha ya kuongezeka kwa uwakilishi wao katika baadhi ya vyombo vya maamuzi.
Kwa mujibu wa takwimu za kimataifa zilizowasilishwa katika maelezo ya jukwaa hilo, wanawake wanachukua takribani asilimia 26 ya viti vya mabunge duniani, lakini bado wanakabiliwa na vikwazo vya kimuundo na kitaasisi vinavyoweza kukatiza safari zao za uongozi.
Changamoto hizo zinaonesha umuhimu wa kuwa na mifumo inayowasaidia wanawake si tu kupata nafasi za uongozi, bali pia kuendelea kushikilia nafasi hizo na kutekeleza majukumu yao kwa muda mrefu.
Katika jukwaa hilo, washiriki pia walipata fursa ya kufahamu matokeo ya awali ya utafiti wenye mada isemayo *“Njia Imara za Uongozi: Kuchunguza Namna ya Kuingia na Kudumu katika Uongozi wa Wanawake nchini Tanzania.”*
Utafiti huo unalenga kuchunguza namna wanawake wanavyoingia katika nafasi za uongozi na mambo yanayochangia au kuzuia udumishaji wao katika nafasi hizo, huku jukwaa likitoa nafasi ya kujadili mapendekezo ya suluhisho za vitendo.
Jukwaa la Uongozi wa Wanawake 2026 limekuwa sehemu ya majadiliano kuhusu umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kuwaendeleza wanawake viongozi, kupanua fursa za kujifunza na kujenga mazingira yanayowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika uongozi katika sekta mbalimbali.

