Afisa Mkuu wa Yas Business, Norman Kiondo (wa pili kushoto), akimpongeza Msimamizi wa Duka la Yas la Michenzania Mall, Bi. Ellen Tumaini Mbwambo, kwa kutambuliwa kuwa miongoni mwa wafanyakazi vinara wa huduma kwa wateja kwa mwaka 2026, katika hafla ya kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa juma. Hafla hiyo ililenga kuthamini mchango wa wafanyakazi katika kuwasaidia wateja na kutatua changamoto za huduma.

……….. 

Dar es Salaam.

Kampuni ya mawasiliano ya Yas imewatambua wafanyakazi waliofanya vizuri katika kutoa huduma kwa wateja kwa mwaka 2026, huku ikisisitiza umuhimu wa mafunzo ya mara kwa mara ili kuimarisha uwezo wao wa kutatua changamoto za wateja.

Hafla hiyo imefanyika mwishoni mwa juma jijini Dar es Salaam, ikiwa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja. Ikilenga kuthamini mchango wa watoa huduma katika kuwasaidia wateja na kushughulikia changamoto zinazowakabili.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Yas, Mwangaza Matotola, amesema ukuaji wa sekta ya mawasiliano na mabadiliko ya teknolojia yanahitaji wahudumu kuendelea kuongezewa ujuzi ili kuwahudumia vizuri wateja wa Yas na Mixx.

Matotola amesema, ingawa huduma kwa wateja imepiga hatua ikilinganishwa na miaka iliyopita, bado kuna haja ya kuimarisha mafunzo ili wahudumu waweze kukabiliana na changamoto mpya zinazoibuka.

Amesema maendeleo ya teknolojia yameleta manufaa kwa watumiaji, lakini pia yameibua changamoto zinazohitaji wahudumu kuwa na uelewa wa kutosha wa huduma za Yas na Mixx pamoja na mabadiliko yake.

Kwa upande wake, Anna Kulinganila, mmoja wa wafanyakazi waliotambuliwa kwa kufanya vizuri katika huduma kwa wateja, amesema kumekuwa na mabadiliko katika namna wateja wanavyowasiliana na wahudumu wanapohitaji msaada.

Amesema simu zenye matusi na lugha zisizo na staha zimepungua ikilinganishwa na miaka iliyopita, ingawa bado wanakutana na baadhi ya wateja wanaotumia lugha isiyofaa.