Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), Dkt. Bill Kiwia akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumamosi, Oktoba 10, 2026, katika ofisi za Bodi Temeke jijini Dar es Salaam. 
…………
Na Mwandishi wetu , Dar es Salaam
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imepanga mikopo na ruzuku yenye thamani ya Shilingi bilioni 535.7 kwa wanafunzi 165,775 katika awamu ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumamosi, Oktoba 10, 2026, katika ofisi za Bodi hiyo zilizopo Tazara Vetenary, Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema fedha hizo zitanufaisha wanafunzi wa shahada ya awali, stashahada, wanaoendelea na masomo pamoja na wanaofadhiliwa kupitia Samia Scholarship.
Dkt. Kiwia amesema kati ya wanufaika hao, wanafunzi 74,769 wa mwaka wa kwanza wa shahada ya awali wamepangiwa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 246.88, huku wanafunzi 8,538 wa stashahada wakipangiwa mikopo ya Shilingi bilioni 22.9.
Amesema wanafunzi wengine 873 wa mwaka wa kwanza wanaofadhiliwa kupitia Samia Scholarship wamepangiwa ruzuku yenye thamani ya Shilingi bilioni 4.5.
Kwa upande wa wanafunzi wanaoendelea na masomo, Dkt. Kiwia amesema wanafunzi 79,115 wa shahada ya awali wamepangiwa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 252.4.
Aidha, amesema wanafunzi 1,554 wa stashahada wanaoendelea na masomo wamepangiwa mikopo ya Shilingi bilioni 3.8, huku wanafunzi 926 wanaoendelea kunufaika na Samia Scholarship wakipangiwa ruzuku yenye thamani ya Shilingi bilioni 5.1.
Amesema upangaji huo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuhakikisha wanafunzi wenye sifa wanapata mikopo na ruzuku kwa ajili ya kugharamia masomo yao katika vyuo mbalimbali nchini.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiwia amewataka waombaji ambao hawakupangiwa mikopo au ruzuku katika awamu ya kwanza kuendelea kufuatilia taarifa za maombi yao kupitia Mfumo wa Maombi na Usimamizi wa Mikopo kwa Wanafunzi (SIPA), wakati uchambuzi na upangaji wa awamu zinazofuata ukiendelea.
Amesema kutopangiwa mkopo au ruzuku katika awamu ya kwanza hakumaanishi kuwa waombaji hao wamekosa nafasi moja kwa moja, kwani Bodi inaendelea na taratibu za uchambuzi na upangaji wa mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Kwa mwaka wa masomo 2026/2027, Serikali imetenga jumla ya Shilingi trilioni 1.06 kwa ajili ya mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Kwa mujibu wa taarifa ya HESLB, bajeti hiyo inalenga kugharamia wanafunzi 292,463, wakiwemo wanafunzi 111,342 wa mwaka wa kwanza wa shahada ya awali.
Vilevile, bajeti hiyo inalenga kugharamia wanafunzi 24,978 wa stashahada, wakiwemo wanafunzi 14,000 wa mwaka wa kwanza, pamoja na wanafunzi 2,738 wa shahada ya awali wanaofadhiliwa kupitia Samia Scholarship, wakiwemo wanafunzi wapya 1,000.
Aidha, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya wanafunzi 513 wa Stashahada ya Juu ya Sheria kwa Vitendo, wakiwemo wanafunzi wapya 350.

