Na Mwandishi Maalumu – Mwanza

10/10/2026 Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) inashiriki katika kambi maalumu ya madaktari bingwa na bobezi inayofanyika katika viwanja vya Nyamagana jijini Mwanza, kwa kutoa huduma za uchunguzi wa awali wa saratani na elimu kwa wananchi ili kuwawezesha kutambua viashiria vya ugonjwa huo na kuchukua hatua stahiki mapema.

Kambi hiyo ilizinduliwa rasmi jana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Kamishna wa Polisi (CP) Salum Hamduni  ikiwa na lengo la kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kuongeza fursa ya kupata huduma za afya kutoka kwa wataalamu mbalimbali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo CP. Hamduni alisema sekta ya afya ina jukumu muhimu la kuhakikisha afya za wananchi zinaimarika kwa kuwapatia huduma bora na kuwaelimisha kuhusu magonjwa mbalimbali  ili waweze kujikinga na kutafuta matibabu kwa wakati.

Alisisitiza kuwa wataalamu wa afya wanapaswa kuwahudumia wagonjwa kwa upendo, uvumilivu na kujituma huku akieleza kuwa wananchi wanahitaji huduma zinazozingatia mahitaji yao ya kiafya na kuwapa matumaini wanapokabiliana na changamoto za afya.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya. Miongoni mwa uwekezaji huo ni kuwaendeleza wataalamu wa afya katika ngazi za ubingwa na ubingwa bobezi pamoja na ujenzi wa wodi ya saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando jijini Mwanza,” alisema CP. Hamduni.

Mkuu huyo wa mkoa aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika kambi hiyo ili kupima afya zao na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu. Pia aliwataka kujiunga na mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuongeza fursa ya kupata huduma za matibabu wanapozihitaji.

Kwa upande wake  Mratibu wa kambi hiyo na Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Mhe. John Nzilanyingi alisema kambi hiyo inatoa huduma mbalimbali za kibingwa za uchunguzi na matibabu zikiwemo za saratani, mifupa, ubongo, mishipa ya fahamu na macho pamoja na huduma nyingine za afya. Alisema huduma hizo zimechangia mwitikio mkubwa wa wananchi wanaojitokeza kupata matibabu.

Akizungumzia ukubwa wa kambi hiyo, Mhe. Nzilanyingi alisema imepangwa kuhudumia wananchi 10,000 katika siku nne sawa na watu 2,500 kwa siku. Aliwataka wananchi kuwa wavumilivu na kufuata utaratibu uliowekwa ili kurahisisha utoaji wa huduma na kuhakikisha kila mmoja anapata huduma inayohitajika.

Naye Meneja wa Huduma za Saratani na Elimu kwa Umma wa ORCI, Dkt. Maguha Stephano alisema taasisi hiyo imejipanga kutoa huduma za uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi, saratani ya matiti na saratani ya tezi dume pamoja na kutoa elimu kuhusu saratani.

Dkt. Maguha alifafanua kuwa wananchi watakaobainika kuwa na viashiria vinavyohitaji uchunguzi au matibabu zaidi watapewa rufaa kwa hatua zinazofuata ili kuhakikisha wanapata huduma kulingana na mahitaji yao ya kiafya.

Ushiriki wa ORCI katika kambi hiyo ni sehemu ya jitihada za kusogeza huduma za uchunguzi wa saratani karibu na wananchi, kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa huo na kuhamasisha uchunguzi wa mapema.

Mwisho

**********************************************************************************************************************************************************************************************************

Picha no. 1 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Kamishna wa Polisi (CP) Salum Hamduni, akipokea zawadi kutoka kwa Meneja wa Huduma za Saratani na Elimu kwa Umma wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dkt. Maguha Stephano wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi wa afya inayofanywa na madaktari bingwa na bobezi katika viwanja vya Nyamagana jijini Mwanza.

Picha no. 2 Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Rehema Nkomola akitoa elimu kuhusu saratani kwa mkazi wa Mwanza aliyejitokeza kupata huduma za uchunguzi wa saratani katika kambi maalumu ya uchunguzi wa afya inayofanywa na madaktari bingwa na bobezi katika viwanja vya Nyamagana jijini Mwanza.

Picha no. 3 Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Jubilate Lauwo akipokea zawadi kutoka kwa Meneja wa Huduma za Saratani na Elimu kwa Umma wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Maguha Stephano wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi wa afya inayofanyika katika viwanja vya Nyamagana jijini Mwanza.

Picha no. 4 Mkazi wa Mwanza akiuliza swali kuhusu saratani wakati wa utoaji wa elimu kwa umma iliyokuwa inatolewa na wataalamu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) katika kambi maalumu ya uchunguzi wa afya inayofanyika  viwanja vya Nyamagana jijini Mwanza kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa huo na umuhimu wa uchunguzi wa mapema.