Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Oktoba 10, 2026
MEYA Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani, Dkt. Nicas Mawazo, amewataka wawekezaji katika manispaa hiyo kushirikiana na Serikali kuchangia maendeleo ya jamii zinazowazunguka, hususan katika kuboresha miundombinu ya elimu na huduma nyingine za kijamii.
Ametoa wito huo wakati wa ziara ya kutembelea viwanda vya Qounquer Investment Company Ltd, kinachozalisha tishu, na Ufresh Food Ltd, kinachozalisha juisi, vilivyopo Kata ya Kongowe, ambapo amesema baadhi ya shule, ikiwemo Sekondari ya Mwambisi, zinakabiliwa na changamoto zinazohitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali kuzitatua.
Dkt. Mawazo amesema Serikali inaendelea kutekeleza wajibu wake katika kuboresha elimu, lakini wazazi, walezi, jamii na wawekezaji wanapaswa kuunga mkono juhudi hizo ili wanafunzi wapate elimu katika mazingira bora.
“Serikali inatekeleza sehemu yake, jamii, wazazi na walezi nao wanapaswa kuchangia, wawekezaji wanapaswa kurudisha kwa jamii kwa kusaidia shughuli za maendeleo, kuboresha miundombinu ya elimu,” alieleza Mawazo.
Amesisitiza umuhimu wa watendaji na wenyeviti wa mitaa na kata kusimamia usafi wa mazingira, huku akivitaka viwanda kuhakikisha vina mifumo bora ya maji taka ili kuzuia uchafuzi wa mazingira na usumbufu kwa wananchi wanaoishi maeneo ya jirani.
Kwa upande wake, Ofisa Masoko na Mahusiano wa Qounquer Investment Company Ltd, Robert Baclay, ameeleza kiwanda hicho kinachangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa bweni la Shule ya Sekondari ya Mwambisi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Baclay amebainisha, kiwanda hicho kinaahidi kushughulikia changamoto zinazohusiana na mfumo wa maji ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi wanaoishi maeneo yanayokizunguka.
Ameeleza kuwa kiwanda hicho kina mpango wa kuachana na matumizi ya kuni na kutumia nishati safi, hatua inayolenga kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo.
Akizungumzia changamoto ya maji yanayotoka kiwandani, mmoja wa wananchi wanaoishi jirani na kiwanda hicho, Samwel Raphael, amesema ni muhimu kuwekwa kwa mifumo bora ya maji taka ili kuzuia maji hayo kusambaa katika maeneo ya makazi na kusababisha usumbufu kwa wananchi.
Naye Mdhibiti Ubora wa kiwanda cha Ufresh Food Ltd, Noela Ngusa, ameelezea awali kulikuwa na changamoto katika mfumo wa maji taka na matibabu yake, lakini wamefanya marekebisho ili kuhakikisha maji yanatibiwa kabla ya kutolewa nje ya kiwanda.
Ngusa amesema kampuni hiyo pia inachangia mabati 500 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la Shule ya Sekondari ya Mwambisi, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuboresha miundombinu ya elimu.
Kwa upande wake, Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Kibaha, Byson Mpogoza, amefafanua viwanda vinapaswa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, Sura ya 191, pamoja na kanuni zinazohusika katika kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
Amesema kifungu cha 144 cha sheria hiyo kinaeleza kuhusu kuwekwa kwa viwango vya utoaji wa maji taka katika vyanzo vya maji, hatua za kuyatibu kabla ya kuingizwa katika mifumo ya majitaka na masharti ya matibabu yanayotakiwa kwa viwanda kabla ya kuyatoa maji hayo kwenye mazingira.
Mpogoza amesisitiza umuhimu wa viwanda kuzingatia matakwa hayo ili kuhakikisha shughuli zao haziathiri afya za wananchi wala mazingira yanayowazunguka.

