Mkurugenzi Msaidizi Sanaa za Ufundi kutoka BASATA, Bona Masenge, akizungumza kwenye tamasha hilo jijini Arusha .

Baadhi ya sanaa za mikono zinazoonyeshwa katika tamasha hilo katika viwanja vya General Tyre jijini Arusha

…………… 

Happy Lazaro ,Arusha.

Arusha. Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii na wadau wa sanaa za ufundi nchini kuhakikisha wanajisajili rasmi ili kunufaika na fursa mbalimbali pamoja na huduma za kitaalamu zinazotolewa na Baraza hilo.

Akizungumza jijini Arusha, Mkurugenzi Msaidizi Sanaa za Ufundi kutoka BASATA, Bona Masenge, amesema Baraza hilo lipo katika tamasha la Arusha Artisan Festival linaloendelea katika viwanja vya General Tyre jijini Arusha yakiwashirikisha wasanii wa kazi za mikono kutoka maeneo mbalimbali Tanzania na nje ya nchi.

Amesema waandaaji wa maonesho hayo walifuata taratibu zinazotakiwa kwa kufika BASATA kwa ajili ya kutambuliwa na kupata vibali, hatua iliyowezesha Baraza hilo kushirikiana nao katika kutoa miongozo ya uendeshaji wa shughuli za sanaa.

Masenge amefafanua kuwa, ushiriki wa BASATA katika maonesho hayo umejikita pia katika kutoa elimu kwa wasanii kuhusu urasimishaji wa shughuli zao, usajili na umuhimu wa kuwa sehemu ya mfumo rasmi wa wasanii nchini.

“Katika siku za maonesho hayo, BASATA imekutana na wadau mbalimbali ili kuelewa shughuli wanazofanya na kuwafafanulia taratibu zinazopaswa kufuatwa katika kuendesha shughuli za sanaa kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.”amesema Masenge .

Ameongeza kuwa Oktoba 8, BASATA iliendesha warsha maalumu iliyowakutanisha wasanii wa Arts and Crafts waliopo kwenye mabanda ya maonesho hayo, ambapo walipata fursa ya kuuliza maswali na kujadili kwa kina masuala yanayohusu usajili na urasimishaji.

Masenge amesema BASATA imewafahamisha wasanii kuhusu mfumo wa AMIS unaowawezesha kujisajili wenyewe, huku akisisitiza kuwa mwombaji anatakiwa kuwa na nyaraka muhimu, ikiwemo namba ya NIDA na TIN, ili kukamilisha taratibu za usajili.

Masenge ameongeza kuwa,msanii anayekamilisha taratibu hizo hutambulika rasmi na BASATA, jambo linalomwezesha kupata huduma na fursa mbalimbali zinazotolewa na Baraza hilo kwa ajili ya kukuza na kuendeleza sanaa nchini.

Ameongeza kuwa,usajili pia ni sehemu ya matakwa ya kisheria, ambapo kanuni za BASATA zilizotolewa Mei 2026 zinamtaka kila mtu anayejihusisha na shughuli za sanaa kuhakikisha anasajiliwa na Baraza hilo.

Amesema BASATA, mbali na kusimamia shughuli za sanaa nchini, hutoa ushauri wa kitaalamu na kisheria kwa wasanii waliosajiliwa, hususan wanapohitaji kuingia katika mikataba na wazalishaji au wadau wengine katika shughuli zao.

“Kupitia dawati la sheria, msanii aliyesajiliwa anaweza kupata ushauri wa kisheria bila gharama, huku Baraza likiendeleza pia huduma ya kuwaunganisha wasanii na fursa mbalimbali kupitia mitandao yake ndani na nje ya nchi.”amesema Masenge .

Ameongeza kuwa , BASATA itaendelea kushirikiana na waandaaji wa matukio ya sanaa pamoja na wasanii ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa rasmi, inalindwa na inakuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.