Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu. 

……………. 

Na Mwandishi Wetu, Arusha

RAIS wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, ametoa wito kwa mabunge duniani kuimarisha sheria, kuongeza uwekezaji na kuweka mifumo madhubuti ya uwajibikaji katika kuhakikisha wanawake, watoto na watoto wachanga wanapata huduma bora za afya.

Akizungumza katika mazungumzo ya pamoja ya kibunge kuhusu afya ya uzazi, mama na mtoto yaliyofanyika Arusha sambamba na Mkutano wa 153 wa IPU, Dkt. Tulia alisema afya ya wanawake, watoto, watoto wachanga na vijana si suala la afya pekee, bali ni suala la haki za binadamu, usawa, maendeleo na utulivu wa taifa.

Dkt. Tulia alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali ya Tanzania, Bunge la Tanzania na wananchi kwa ukarimu wao na kwa kuwezesha mazingira mazuri ya kufanyika kwa mkutano huo muhimu wa kimataifa wa mabunge.

Alisema uongozi na dhamira ya Rais Samia vimechangia kuileta pamoja jumuiya ya wabunge duniani katika mkutano huo, huku akieleza kuwa uongozi wake umeendelea kusukuma mbele ajenda ya kuboresha afya na ustawi wa jamii, kuimarisha mifumo ya afya pamoja na kuhakikisha uwekezaji endelevu na uwajibikaji katika sekta hiyo.

Kwa mujibu wa Dkt. Tulia, wabunge wana nafasi muhimu ya kutunga sheria zinazolinda afya na haki za wanawake na watoto, kutenga rasilimali zinazohitajika, kusimamia matumizi yake na kuhakikisha Serikali zinawajibika katika utoaji wa huduma hizo.

Alisema ni muhimu ahadi za kisiasa ziwekwe kwenye bajeti kwa kuwekeza katika huduma za afya ya msingi, huduma za afya ya mama na mtoto mchanga, lishe pamoja na dawa muhimu za kuokoa maisha.

Dkt. Tulia pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi na uwajibikaji, akisema takwimu na ushahidi wa kuaminika vinahitajika ili kubaini maeneo yenye ukosefu wa usawa na kuhakikisha wanawake, vijana na jamii wanashirikishwa katika maamuzi yanayohusu maisha yao.

Aidha, aliwataka wabunge kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu, suluhisho na mbinu bora kati ya mabunge ili kutafsiri ahadi za kimataifa kuwa vipaumbele vya kitaifa na matokeo yanayopimika.

Dkt. Tulia alisema IPU imejizatiti kuwa mshirika wa vitendo kwa mabunge katika kuimarisha uwezo wa kutunga sheria madhubuti za afya, kuandaa na kusimamia bajeti, kufanya uangalizi na kudai uwajibikaji, huku akisisitiza umuhimu wa kuwawezesha wabunge kuwa na zana, ushahidi, ushirikiano na mifumo ya uwajibikaji.

Alisema lengo linapaswa kuwa kutoka kwenye ahadi kwenda utekelezaji, kutoka utekelezaji kwenda uwajibikaji na kutoka uwajibikaji kwenda kwenye matokeo, akisisitiza kuwa hakuna muda wa kuchelewesha hatua za kukabiliana na vifo na madhara yanayoweza kuzuilika.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, alisema ni heshima na fursa kubwa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo muhimu ya pamoja ya kibunge yanayolenga kuimarisha uongozi katika masuala ya afya ya wanawake, akina mama, watoto, watoto wachanga na vijana.

Spika Zungu alisema afya ya wanawake, akina mama, watoto, watoto wachanga na vijana si suala la afya pekee, bali linahusiana pia na haki za binadamu, usawa, maendeleo na utulivu wa taifa, akisisitiza kuwa huduma muhimu za kuokoa maisha, ikiwemo dawa za kudhibiti na kuzuia kuvuja damu wakati wa kujifungua, zinahitaji kuwekwa katika vipaumbele vya ufadhili.

Spika Zungu pia alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna alivyotoa uongozi na kujitoa katika kuhakikisha huduma za afya ya mama na mtoto zinaendelea kuboreshwa nchini, akisema juhudi hizo ni sehemu muhimu ya kuimarisha afya na ustawi wa wanawake na watoto Tanzania.