Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeandika historia katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini baada ya kunyakua tuzo ya mshindi wa kwanza kwa taasisi za Elimu zilizokuwa zikishiriki katika maonesho hayo.Tuzo za washindi zimetolewa leo, tarehe 2 Oktoba 2026 na Dkt. Latifa Hamis Mohamed, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano). 

Mshindi wa pili katika kundi hilo ni Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na wa tatu ni Chuo cha Sayansi ya Afya Shinyanga. 

Katika maonesho hayo ya madini yaliyoanza tarehe 23 Septemba katika viwanja vya Dkt Samia Suluhu Hassan, Bombambili Geita, VETA ilitumia maoneshoa hayo kutangaza mafunzo yanayohusiana na sekta ya madini, kuonesha ubunifu na teknolojia zilizobuniwa na wakufunzi na wanafunzi wa VETA kwa ajili ya kutatua changamoto zinazohusiana na uchumi wa Kanda ya Ziwa.

Meneja Uhusiano kwa Umma na Masoko Sitta Peter amesema ushindi huo ni kielelezo cha juhudi zinazofanywa na Mamlaka hiyo katika sekta ya madini na nyanja zingine za kiuchumi.