Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema Serikali imepokea na kufanyia kazi malalamiko ya madereva wa mabasi ya masafa marefu, huku akitangaza hatua mbalimbali za kutatua changamoto zinazowakabili, ikiwamo mfumo wa VTS, kufungiwa kwa leseni na usimamizi wa askari wa usalama barabarani.

Katambi ameyasema hayo leo Septemba 30,2026 katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Dar es Salaam, wakati akizungumza na madereva baada ya mgomo uliosababisha usafiri wa mabasi ya mikoani kusimama, akieleza kuwa Serikali imeanza kupitia hoja zote zilizowasilishwa na viongozi wa madereva na baadhi tayari zimefanyiwa uamuzi.

Alisema baadhi ya masuala yalihitaji uamuzi wa kiutawala, mengine kisheria na mengine vikao vya pamoja vya Serikali, akibainisha kuwa hoja zilizojadiliwa na madereva zimefikishwa kwa viongozi wakuu wa Serikali kwa ajili ya hatua zaidi.

Kuhusu madereva ambao leseni zao zilifungiwa au kufutwa, Katambi alisema Serikali inaendelea kuchambua kesi hizo dereva kwa dereva na barua kwa barua, ili kutoa nafuu kwa wale ambao makosa yao hayakuwa na madhara makubwa, bila kuingilia kesi ambazo zimehusisha uzembe mkubwa, ulevi au kusababisha vifo.

Alisema Baraza la Taifa la Usalama Barabarani linaendelea na uchambuzi huo na ndani ya siku chache Serikali itatoa maamuzi kwa umma kuhusu madereva watakaonufaika na msamaha au nafuu, akisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuwawezesha kurejea kazini na kushiriki katika ujenzi wa uchumi.

Kuhusu mfumo wa VTS, Katambi alisema Serikali imepokea malalamiko na ushahidi unaoonyesha kuwepo kwa changamoto katika baadhi ya mifumo hiyo, ikiwamo tofauti kati ya taarifa za kamera za trafiki na usomaji wa VTS, hivyo Wizara ya Mambo ya Ndani, Uchukuzi, Ujenzi pamoja na Kazi zitatakiwa kukutana na kutafuta utaratibu bora.

Alisema Serikali inapanga kutumia teknolojia ya kisasa ya kamera katika udhibiti wa mwendo wa magari, akifananisha mfumo huo na VAR inayotumika katika soka, ili kuhakikisha madereva hawapewi adhabu kwa upendeleo au kuonewa na kwamba taarifa za makosa zinakuwa na ushahidi wa moja kwa moja.

Aidha, Katambi alikataza utaratibu wa askari kuwavizia madereva barabarani kwa lengo la kuwakamata, akisema Jeshi la Polisi limeagiza kuwa magari yanayokiuka sheria yatatambuliwa na kufuatiliwa kwa kutumia mifumo iliyopo, huku viongozi wa usalama barabarani wakisimamia utekelezaji huo.

Alisema Serikali pia itajadili namna ya kuwapatia madereva mafunzo ya uongezaji wa ujuzi bila kuwaondoa kwenye ajira kwa muda mrefu, huku ikipitia utaratibu wa mafunzo kupitia VETA, Jeshi la Polisi na taasisi nyingine ili kuhakikisha madereva wanakuwa na uwezo unaokidhi viwango vya usalama barabarani.

Katika hatua nyingine, Katambi alisema Serikali itawataka waajiri kuhakikisha madereva wanapewa mikataba ya ajira inayoeleza haki zao za msingi, ikiwamo masuala ya mafao na michango ya mifuko ya hifadhi ya jamii, huku akisema suala la faini na taratibu nyingine za LATRA litajadiliwa katika kikao cha pamoja cha Serikali.

Awali, Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva Tanzania (WAMATA), Mnajwa Kafumu, aliomba radhi kwa abiria waliokwama kutokana na mgomo huo na kuwataka madereva kurejea kazini kwa weledi, wakizingatia sheria za usalama barabarani na kuhakikisha abiria wanafika salama, huku Mwenyekiti wa Taasisi ya Kutetea Taaluma ya Madereva Tanzania, Yohana Mwenyegera, akiwasihi madereva kutumia mazungumzo na Serikali kutatua changamoto badala ya migomo.

Mapema kabla ya kwenda kituoni hapo Katambi alifanya mazungumzo na baadhi ya madereva na viongozi wao kisha baadae wakaongozana kwenda kufanya mazungumzo na Waziri mkuu na kufikia muwafaka wa kumaliza mgogoro huo.