Helsinki, Finland
Tanzania imeweka wazi dhamira yake ya kubadili Sekta ya Madini kutoka utegemezi wa uchimbaji na uuzaji wa malighafi kuelekea kujenga mnyororo shindani wa thamani unaojumuisha uchakataji, usafishaji, utengenezaji na uuzaji wa bidhaa zenye thamani kubwa.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, wakati akizungumza Septemba 28, 2026, jijini Helsinki, Finland, katika Jukwaa la Uwekezaji na Biashara kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania, ambapo amesema Tanzania ina fursa kubwa ya kuwa sehemu muhimu ya minyororo ya kimataifa ya thamani ya madini kutokana na utajiri wake wa dhahabu, almasi, tanzanite, ruby, sapphire, tsavorite na zircon, pamoja na madini muhimu na ya kimkakati kama graphite, nickel, madini adimu ya ardhini (REE), uranium, copper na lithium.
Mbibo amesema Serikali inatafuta wawekezaji ambao hawataishia kwenye uchimbaji pekee, bali watakaokuja na mtaji, teknolojia, utaalamu na upatikanaji wa masoko ya kimataifa kwa ajili ya kujenga shughuli za uchakataji, usafishaji, utengenezaji, miundombinu, huduma za kitaalamu na biashara zinazohusiana na madini. Miongoni mwa miradi yenye fursa za uwekezaji ni Kabanga Nickel, Ngualla Rare Earth, miradi ya graphite Mahenge na Lindi pamoja na Sotta Uranium, sambamba na fursa nyingine katika dhahabu, shaba, lithium na vito.
Amesema Tanzania inaendelea kujenga mazingira wezeshi ya uwekezaji kupitia sera na sheria zinazotabirika, mifumo rasmi ya makubaliano, miundombinu inayoboreshwa na mfumo wa kikodi wenye vivutio kwa wawekezaji. Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha nishati, reli, barabara, viwanja vya ndege na bandari ili kusaidia shughuli za uzalishaji, uchakataji na biashara katika sekta ya madini.
“Sekta ya Madini ilichangia asilimia 10.3 ya Pato la Taifa mwaka 2025 na inachangia zaidi ya asilimia 50 ya mapato ya mauzo ya nje ya Tanzania. Utajiri huu wa madini unatoa nafasi kwa taifa kuongeza mapato, ajira, uwekezaji wa kigeni na kuchochea viwanda,” amesema Mbibo, akisisitiza kuwa uongezaji thamani, uchakataji na usafishaji wa madini ni muhimu katika kuhakikisha Tanzania inabaki na sehemu kubwa zaidi ya thamani inayotokana na rasilimali zake” amesema Mbibo.
Mbibo amewaalika wawekezaji, Kampuni za madini, taasisi za fedha, watoa teknolojia na wadau wengine wa sekta hiyo kushiriki katika Mkutano wa 7 wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania (TMIC 2026), unaotarajiwa kufanyika Novemba 19–21, 2026 jijini Dar es Salaam. Amesema mkutano huo utatoa fursa kwa washiriki kujadili kwa kina fursa za uwekezaji, kushirikishana teknolojia na utaalamu, pamoja na kujenga ushirikiano wa muda mrefu katika uchimbaji, uchakataji, uongezaji thamani na uendelezaji wa madini nchini.
Katika kuainisha fursa zilizopo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Eng. Ally Samaje, amesema maeneo mbalimbali nchini yana uwezo mkubwa wa uwekezaji katika madini ya kimkakati yakiwemo nickel, copper, cobalt, rare earth elements, tin, tungsten, gold, PGM, uranium, graphite, lithium, iron ore, helium, hydrogen, titanium minerals na heavy minerals. Amesema Serikali inalenga kuongeza utafiti wa kijiolojia kwa kutumia teknolojia ya High-Resolution Airborne Geophysical Survey, kutoka asilimia 16 ya eneo lililofanyiwa utafiti hadi asilimia 50 ifikapo mwaka 2030, huku utafiti wa kijiokemia ukilenga kuongezeka kutoka asilimia 24 hadi asilimia 50.

