Consolatha Mmbando, Chunya, Mbeya
Wananchi mkoani Mbeya wanaendelea kupata huduma kwenye Kliniki ya Ardhi Kidjiti inayoendelea wilayani Chunya, ambapo jumla ya wananchi 227 wamepata huduma, Hatimiliki 120 zimesajiliwa huku Hati 57 zikitolewa kwa wananchi.
Kwa upande wa mapato, mkoa wa Mbeya kwa kipindi cha kuanzia Septemba 21 hadi 25, 2026, kliniki hiyo imekusanya zaidi ya shilingi milioni 74 kutokana na huduma mbalimbali za ardhi zinazotolewa kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza mapato ya Serikali yanatokanayo na Sekta ya Ardhi.
Malengo mengine ya Kliniki hiyo ni pamoja na kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi, kutoa elimu na ushauri kuhusu masuala ya ardhi pamoja na kusaidia wananchi kutatua changamoto zinazohusiana na ardhi kwa wakati.
Kliniki ya Ardhi inafanyika kwa wakati mmoja katika mikoa yote ya Tanzania Bara kuanzia Septemba 22, 2026. Kliniki hiyo ilizinduliwa rasmi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, Septemba 25, 2026, mkoani Mtwara, na inatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 3, 2026, ikiwa na kaulimbiu isemayo “Kliniki ya Ardhi Kidijiti, e-Ardhi Huduma Popote.”
Akizungumza kuhusu mwitikio wa wananchi, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mbeya Bi. Syabumi Mwaipopo amesema mwitikio wa wananchi wa Wilaya ya Chunya ni mkubwa, huku akibainisha kuwa wananchi wengi hufika kupata huduma nyakati za asubuhi na jioni kutokana na shughuli zao za uchimbaji wa madini zinazowafanya kuwa na muda mchache wakati wa mchana.
“Tumepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi wa Chunya katika kliniki hii ya ardhi. Wananchi wengi wamekuwa wakifika kupata huduma nyakati za asubuhi na jioni kutokana na shughuli zao za uchimbaji wa madini, ambazo huwafanya kuwa na muda mchache wakati wa mchana,” amesema Mwaipopo.
Kliniki ya Ardhi katika Mkoa wa Mbeya inafanyika kwa wakati mmoja katika maeneo ya Matundasi, Makongolosi na Itumbi, wilayani Chunya. Hatua hiyo inalenga kuboresha utoaji wa huduma za ardhi na kuhakikisha wananchi wanazipata kwa urahisi na ufanisi na hivyo kuleta tija kwa wananchi na kuwapatia tabasamu.
Kwa upande wake mkazi wa Chunya Bw. Oscar Mpangala ameishukuru serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuanzisha mfumo wa e-Ardhi ambao umerahisisha upatikanaji wa huduma za ardhi kwa wananchi.
“Nashukuru Wizara imerahisisha sana, kwahiyo niwasihi wananchi pia na nyie mjitokeze kwa wingi, hakuna usumbufu kila kitu kinakua kiurahisi na kiko wazi”. Amesema Mpangala.

