WANANCHI wa Bumbwini, Zanzibar, wamewaomba Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kumuuliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuhusu hatima ya mashamba yao, mazao na vilimo vinavyodaiwa kuharibiwa katika maeneo yanayotengwa kwa ajili ya uwekezaji na miradi ya maendeleo.
Wananchi hao wametoa ombi hilo leo, tarehe 23 Septemba 2026, mbele ya ujumbe wa viongozi wa ACT Wazalendo, ukiongozwa na Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi kupitia chama hicho Pro. Omar Fakih Hamad wakiwa katika ziara maalum ya kusikiliza kero zinazowakabili wananchi wa maeneo mbali mbali Zanzibar.
Walisema hawapingi maendeleo wala uwekezaji, lakini wanataka haki zao za ardhi, mazao na fidia zilindwe, huku wakitaka taratibu za kisheria zinazohusiana na utwaaji wa ardhi kwa ajili ya miradi ya maendeleo zifuatwe.
Thuweni Swaleh Mazrui, mkazi wa Kiomba Mvua, alisema wananchi hawapingi maendeleo, lakini ameeleza kutoridhishwa na namna baadhi ya maeneo yao yanavyofanyiwa kazi bila wao kupewa taarifa za kutosha.
“Tuliwazuia wasifanye kazi ile, lakini walisema wao wametumwa na Serikali. Sisi wananchi hatukupata taarifa yoyote,” amesema Thuweni.
Alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakiona maeneo yao yakichukuliwa bila kupata maelezo ya kutosha kuhusu fidia.
“Ardhi zetu zinachukuliwa. Hata kusema watulipe fidia wanasema ni mali ya Serikali. Aaah jamani, hapa kwetu sasa tuende wapi?” amehoji Thuweni
Thuweni ameongeza kuwa wananchi wamekuwa wakiamka na kukuta mitambo ikifanya kazi katika maeneo yao.
“Unaamka alfajiri unakuta maburdoza tu, yanaondoa vipando vyetu.” alieleza Thuweni
Naye Shida Shadhili, mkazi wa Bumbwini, alisema wananchi waliwaomba wahusika wasivuruge maeneo yao kabla ya kulipwa fidia, lakini anadai mazao yaliharibiwa kabla ya malipo kufanyika.
Alisema wananchi pia walikataa kufanyiwa tathmini mpya katika mazingira ambayo, kwa maelezo yake, tathmini ya awali haikufanyika kwa baadhi yao.
“Walipokuja kutaka kutuandika tulikataa, kwa sababu mwanzo hawakutufanyia tathmini. Mpaka tulipwe ya mwanzo, halafu ndiyo tufanyiwe tathmini mpya.”
Shida ameitaka Serikali kuangalia upya hali hiyo, akirejea kauli ya Rais kwamba hakuna mwananchi atakayeadhibiwa au kudhulumiwa.
“Rais wetu alisema hatomdhulumu mtu, leo kwa nini tunadhulumiwa na yeye yupo? Kwani vipi?”
Kwa upande wake, Makame Khamis Salim, mkazi wa Bumbwini Mikweni, alisema wananchi hawakatai kufanyiwa tathmini, lakini wanataka tathmini inayozingatia thamani halisi ya ardhi pamoja na mazao yaliyopo juu yake.
“Hatutakataa kufanyiwa tathmini, lakini tunataka tathmini ambayo na sisi watu wa Bumbwini tutaridhika,” amesema Makame.
Alisema tathmini haipaswi kuangalia zao pekee bila kuzingatia ardhi inayoliwezesha zao hilo kuwepo.
“Unapiga tathmini mnazi, lakini ardhi iliyoshikilia mnazi kwa nini isitathminiwe?”
Makame alisema iwapo wananchi hawapati haki wanayoona inawastahili, wanaona ni bora kupewa fursa ya kushughulikia ardhi zao wenyewe.
“Bora tuachiliwe tuuze wenyewe,” amesema.
Daima Shore amesema wananchi wamekuwa wakipata hasara kutokana na kuondolewa kwa minazi na mazao mengine katika maeneo yao.
“Tunadhalilika kwenye ardhi yetu bila hata kulipwa fidia. Minazi yetu yote imeangushwa.”
Alisema kuondolewa kwa minazi kumeathiri kipato cha familia ambazo zilikuwa zinategemea mazao hayo.
“Wapi tukapate nazo leo, wakati yote imeshakatwa? Kwa hiyo tunalazimishwa tukanunue nazi. Huu ndiyo mkakati wa kupunguza umasikini au kuongeza?”
Kwa mujibu wa Daima, baadhi ya ardhi hizo ni maeneo yaliyorithiwa kutoka kwa wazazi na wazee wao.
Kibadi Khamis Kiate alisema eneo lao limechukuliwa huku wananchi wakidai kutolipwa fidia wala kupewa maelezo ya kutosha kuhusu mchakato huo.
“Tumenyang’anywa eneo letu na hatukulipwa hata senti. Na leo hii meli zinateremsha mafuta, wakati tulionyang’anywa mashamba na kuvurugiwa vipando na vilimo vyetu, hatujalipwa, na hati miliki tunazo.” alisema kibad
Alisema licha ya wananchi kuwa na nyaraka za umiliki, bado wanadai hawajapata tathmini wala malipo wanayodai wanastahili.
“Hata kufanyiwa tathmini hatukufanyiwa, sembuse malipo. Lakini wakubwa husema tayari tumelipwa.” alieleza
Kibadi alisema uwekezaji unaoendelea katika eneo hilo haujawanufaisha kwa namna wanayoitarajia, kutokana na kupoteza mashamba na mazao yao.
“Sijaona faida ya uwekezaji, kwani mashamba na vipando vyangu vimevurugwa, hata kupewa ahsante hatukupewa, wacha fidia. Mashamba yangu manne yote yamevurugwa.”
Amesema pamoja na changamoto hizo, wananchi hawataki kuondoka katika maeneo yao.
“Hatuna pakujenga, lakini tunasema sisi hatuhami. Na aambiwe Rais kuwa sisi hatuhamii.”
Mmanga Hamed Muhammed ambaye ni Mwakilishi wa wananchi Jimbo la Tumbe kupitia Chama cha ACT Wazalendo kwa niaba ya Wawakilishi hao aliwaahidi wananchi hao kuwa kero na matatizo yao watayachukulia khatua za hara ili kujua khatima ya Ardhi na vipando vya vilivyoteketezwa kwa ajili kupisha miradi ya maendeleo.
Naye Mwakilishi wa Ziwani Mohd Ali Salum .wakilishi wa Jimbo Ziwani alimuomba Rais wa Zanzibar kusikiliza vilio vya wananchi wake ambao wanalia kila pembe za Zanzibar juu kukosa fidia za mali na Ardhi zao.
Maeneo ya Bumbwini yamekuwa yakihusishwa na miradi ya uwekezaji na maendeleo, ikiwemo ujenzi wa Bandari Mpya pamoja na ujenzi wa mtambo wa gesi, hali ambayo imeongeza umuhimu wa wananchi kupata ufafanuzi kuhusu maeneo yanayochukuliwa, taratibu zinazotumika na haki zao katika mchakato huo.
Katika ziara hiyo, Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi kupitia ACT Wazalendo aliambatana na Mwakilishi Mtambwe Dk. Muhammed Ali Suleiman, Mwakilishi wa Ole Seif Hamad Suleiman, Mwakilishi wa Ziwani Mohd Ali Salum, Mwakilishi wa Tumbe Mmanga Hamed Muhammed, Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba Moza Muhammed Khamis na Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Kaskazini Pemba Farida Amour Muhammed.

