Mwenyekiti wa wabunge vinara wa ufuatiliaji na tathmini ,Tanzania Chapter,Mhandisi Mwanaisha Ulenge akizungumza kwenye kongamano hilo jijini Arusha leo.


Na Happy Lazaro, Arusha
Mwenyekiti wa wabunge vinara wa ufuatiliaji na tathmini ,Tanzania Chapter,Mhandisi Mwanaisha Ulenge amesema kuwa ,ufuatiliaji na tathmini ni muhimu kuingizwa katika utendaji wa kila siku wa Serikali ili kuhakikisha mipango na shughuli zinazotekelezwa zinatoa matokeo yanayotarajiwa kwa wananchi.
Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza katika kongamano la tano la kitaifa la wiki ya ufuatiliaji na tathmini na ujifunzaji (MEL) linaloendelea katika hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha .
Mhandisi Ulenge ameipongeza Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Bunge kwa kuanzisha Kamati Maalum ya Kudumu ya Bunge ya Ufuatiliaji na Tathmini, iliyotangazwa rasmi Septemba 8 mwaka huu, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Amesema kuwa,kuanzishwa kwa kamati hiyo kunaonyesha dhamira ya Bunge ya kuhakikisha rasilimali za wananchi zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo yenye tija kwa jamii, huku akiwapongeza wabunge kwa kuunga mkono ajenda hiyo.
Aidha, ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na wadau wa ufuatiliaji na tathmini kwa kuandaa Kongamano la Tano la Ufuatiliaji na Tathmini, akisema jukwaa hilo ni muhimu katika kujenga utamaduni mpya wa utendaji wa Serikali unaozingatia ushahidi, matokeo na uwajibikaji.
“Bunge lina wajibu wa kuisimamia Serikali na kuhakikisha rasilimali za wananchi zinatumika kwa ufanisi, hivyo ufuatiliaji na tathmini ni nyenzo muhimu katika kutekeleza jukumu hilo na kufanya maamuzi yanayolenga kuboresha maisha ya wananchi.”amesema Ulenge
“Hatutaangalia tu kama shughuli zimefanyika ipasavyo, tutauliza pia zimeleta matokeo gani chanya kwa wananchi na zimebadilisha nini katika maisha ya wananchi na tumejifunza nini ili kufanya vizuri zaidi. Hapo ndipo nguvu ya ufuatiliaji na tathmini ilipo,” amesema Mhandisi Ulenge .
Ulenge amefafanua kuwa, wabunge wanapaswa kuangalia zaidi matokeo ya mwisho ya miradi na programu kwa wananchi, badala ya kuishia katika kujua kiasi cha fedha kilichotumika au idadi ya shughuli zilizotekelezwa.
Ameongeza kuwa, Tanzania inapotekeleza mipango mikubwa ya maendeleo na kuendelea na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, ni muhimu kuwa na uwezo wa kutambua kinachofanya kazi, kinachohitaji kuboreshwa na sababu za mafanikio au changamoto zinazojitokeza.
Amesema kuwa ,wabunge wamejipanga kuunganisha ushahidi unaopatikana kupitia ufuatiliaji na tathmini na maamuzi ya Bunge, huku wakihimiza matumizi ya ushahidi katika mijadala na usimamizi wa Serikali, pamoja na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji inayozingatia matokeo.
“Wabunge wataendelea kujifunza kutokana na mafanikio na changamoto za utekelezaji wa miradi na programu, huku wakihamasisha matumizi ya ufuatiliaji na tathmini katika kuboresha huduma kwa wananchi.”amesema Mhandisi Ulenge
Amesisitiza kuwa ,ufuatiliaji na tathmini si jukumu la wataalamu wa M&E pekee, bali ni ajenda ya Serikali, Bunge na Taifa kwa ujumla, kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo unaleta matokeo chanya na endelevu kwa wananchi.
Amesema lengo ni kufikia hatua ambapo swali la msingi katika utekelezaji wa mradi au mpango halitakuwa tu kiasi cha fedha kilichotumika, bali pia matokeo yaliyopatikana na namna maisha ya wananchi yalivyoboreshwa.
