Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia Ayubu Charles [36] na Meshack Mwashimala [48] wote wakazi wa Itewe Mkoa wa Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na mali ya wizi shehena ya mbegu za Mahindi zaidi ya tani 15.

Awali Septemba 20, 2026 saa 1:30 asubuhi Wakala wa Mbegu za Serikali [Agricultural Seed Agency – ASA] ilitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Mbeya za kuibiwa mbegu hizo za Mahindi zenye ruzuku ya Serikali mifuko 375. Kufuatilia taarifa hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia Kikosi maalum cha kuzuia na kupambana na uhalifu lilianza ufuatiliaji na majira ya saa 11 jioni lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili wakiwa na shehena hiyo.

Watuhumiwa walikamatwa wakiwa katika Mtaa wa Viwandani, Kata ya Mwakibete, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya wakiwa na shehena hiyo ya mbegu za Mahindi yenye thamani ya shilingi 56,250,000/= mali ya Wakala wa Mbegu za Serikali [ASA] Nyanda za Juu Kusini wakiwa wameficha kwenye Godown la kuhifadhia mizigo mbalimbali.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa wito kwa baadhi ya wananchi kuacha tamaa ya kujipatia fedha kwa njia zisizo halali na badala yake watafute shughuli halali kwa ajili ya kujipatia kipato halali kwani Jeshi la Polisi halitasita kumkamata mtu yeyote na kumchukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

Imetolewa na:
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.