*Ataja umwagiliaji, zana za kisasa za kilimo, na uongezaji thamani kuwa maeneo ya kimkakati
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imedhamiria kuongeza uwekezaji katika maeneo ya umwagiliaji, uzalishaji wa mbegu kwa wingi na matumizi ya zana za kilimo kisasa kama njia ya kuimarisha sekta ya kilimo.
Amesema hayo leo (Jumatatu, Septemba 21, 2026) wakati akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Dkt. Qu Dongyu kuhusu mageuzi ya mifumo ya chakula na kilimo nchini Tanzania, ambako anashiriki Mkutano wa Kimataifa wa Kujadili Afya Moja na Mifumo ya Chakula na Kilimo unaofanyika katika Makao Makuu ya FAO, jijini Roma, Italia.
Dkt. Mwigulu amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeongeza uwekezaji katika kilimo na kuelekeza nguvu katika miradi ya kimkakati, huku ikilenga kuhakikisha wakulima wanapata zana za kilimo na huduma bora zaidi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Amesema Tanzania pia ina fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji kutokana na uwepo wa ardhi nyingi na vyanzo vya maji, hivyo inataka kutumia rasilimali hizo kujenga mifumo ya kilimo inayostahimili mabadiliko ya tabianchi.
“Tanzania inalenga kuacha kuuza bidhaa ghafi, ambazo zimekuwa zikileta changamoto tunapokutana na misukosuko katika masoko ya dunia. Tunataka kuongeza thamani ya mazao na kuwa na masoko yenye ushindani,” amesema.
Waziri Mkuu amesema Tanzania pia inaendelea kutumia teknolojia za kidijitali katika kuwaandikisha wakulima na wasambazaji wa pembejeo, hatua inayosaidia kuboresha usambazaji wa zana za kilimo, mbolea na huduma nyingine kwa wakulima.
Akielezea matarajio ya baadaye katika sekta ya kilimo, Waziri Mkuu amesema Tanzania inataka kuelekeza nguvu katika programu chache za kimkakati zitakazotoa matokeo makubwa na yanayopimika ikiwemo kuhamasisha uwekezaji na mitaji kwa ajili ya mageuzi ya sekta hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Dkt. Qu Dongyu, ameitaka serikali ya Tanzania iwekeze kwa wanasayansi na watafiti chipukizi ili waweze kufanya mageuzi makubwa.
“Wekezeni kwa wanasayansi chipukizi. Muwatajirishe kwa kuwawezesha kushiriki kwenye tafiti na bunifu mbalimbali,” alisisitiza na kuongeza kwamba: “Serbia ilifanya hivyo na ndani ya miaka miwili imefanikiwa kubadilika na kukua kiuchumi ndani ya miaka miwili tu.”
Alisema pamoja na mipango mizuri iliyopo kwenye kilimo, Serikali ya Tanzania isiache kuwashirikisha wakulima wadogo kwenye maamuzi kuhusu masuala yanayowahusu kwani wao ndiyo watekelezaji wakuu.
Dkt. Dongyu amesema FAO pia inaendelea kuhimiza matumizi ya viwango katika uzalishaji na biashara ya mazao, pamoja na matumizi ya teknolojia kuwaunganisha wakulima wadogo na masoko, ili kuongeza ushindani na kunufaika na fursa za biashara.
Dkt. Mwigulu anamwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo wa kimataifa unaofanyika jijini Roma kuanzia Septemba 21 hadi 23, 2026.

