Na Mwandishi wetu, Nzega

MWENGE wa uhuru umezindua mradi wa barabara ya lami ya Lumambo – Kitongo yenye urefu wa kilomita 1.750 iliyopo kwenye Kata ya Nzega Mjini Magharibi Mkoani Tabora.

Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Nzega, mhandisi Haruna Mbagalla, akizungumza kwenye uzinduzi wa barabara hiyo amesema lengo la mradi huo ni kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa na abiria katika mji wa Nzega na vitongoji vyake.

Mhandisi Mbagalla amesema ujenzi wake ulianza Mei 12 mwaka 2024 na unatarajiwa kukamilika Desemba 31 mwaka 2026 chini ya mkandarasi Samota Transport Company LTD.

“Gharama za mradi ni shilingi za kitanzania 1,751,051,480.00 fedha kutoka Serikali kuu,” amesema mhandisi Mbagalla.

Amesema mradi huo utarahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa na abiria mji wa Nzega na vitongoji vyake na kuchochea maendeleo, kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji na kuboresha mandhari ya mji wa Nzega.

Mkuu wa Wilaya ya Nzega Naitapwaki Lemea Tukai ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha za ujenzi na uboreshaji wa barabara za mji wa Nzega.

Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2026 Wazo Michael Mwang’onda amewapongeza TARURA kwa ukamishaji wa barabara hiyo ya lami.

“Pamoja na kuwa barabara hii ipo pembezoni mwa mji wa Nzega ila watu wataitumia na kunufaika nayo ila inavutia na thamani ya fedha inalingana na ubora wake,” amesema Mwang’onda.

Kauli mbiu ya mwenge wa uhuru mwaka 2026 ni Tanzania ni yetu sote Tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo”.