Tanzania itakuwa mwenyeji wa Kongamano la Sita la Jumuiya ya Taasisi za Mitaala Afrika (African Curriculum Association–ACA), litakalofanyika kwa siku nne kuanzia Septemba 22 hadi 25, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 19, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, amesema kongamano hilo limeandaliwa na TET kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Zanzibar (TEZ), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.
Dkt. Komba amesema Tanzania ilitangazwa kuwa mwenyeji wa kongamano hilo wakati wa Kongamano la Tano la ACA lililofanyika Abuja, Nigeria, mwaka 2025, na tangu wakati huo maandalizi ya kitaalamu na kiutendaji yameendelea kufanyika kwa ushirikiano na Jumuiya ya Taasisi za Mitaala Afrika.
Amesema kaulimbiu ya kongamano hilo ni “Transforming Education Systems in Africa: Curriculum Reforms, Teacher Preparation and Inclusive Innovation in the Age of AI and Emerging Technologies,” inayolenga kujadili mageuzi ya mifumo ya elimu, maboresho ya mitaala, maandalizi ya walimu na ubunifu jumuishi katika matumizi ya Akili Unde na teknolojia zinazoibuka.
“Kongamano hili litatoa nafasi ya kujadili namna mitaala ya Afrika inavyoweza kuboreshwa ili kuwa na wahitimu wenye maarifa, umahiri, stadi, maadili na ubunifu unaohitajika katika Karne ya 21,” amesema Dkt. Komba.
Amesema washiriki wa kongamano hilo wanatarajiwa kuwa wakuza mitaala, watafiti wa elimu, wataalamu na wadau wa mitaala, watunga sera, washirika wa maendeleo, walimu na wakufunzi, wahadhiri pamoja na wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu kutoka Tanzania, Afrika na maeneo mengine duniani.
Dkt. Komba amesema kuwa kuwa mwenyeji wa kongamano hilo ni fursa kwa Tanzania kuonesha mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya elimu, ikiwemo maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la Mwaka 2023, pamoja na maboresho ya mifumo na mitaala ya elimu.
Amesema kongamano hilo lina umuhimu wa kimkakati kwa Tanzania kwa kuwa linaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika na Lengo la Nne la Maendeleo Endelevu (SDG 4), vinavyosisitiza umuhimu wa elimu bora na ujenzi wa rasilimali watu yenye ujuzi.
“Ni jukwaa muhimu la kuunganisha watunga sera, watafiti na watekelezaji wa sera ili kupata ushahidi na mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha maamuzi ya kisera kuhusu mitaala, maandalizi na maendeleo ya walimu, mifumo ya tathmini, elimu jumuishi, TEHAMA, Akili Unde na teknolojia nyingine zinazoibuka,” amesema.
Kongamano hilo litahusisha uwasilishaji wa makala 80, majadiliano, maonyesho ya bunifu na teknolojia mbalimbali za kielimu pamoja na ziara ya kielimu ambapo washiriki watapata fursa ya kutembelea mojawapo ya shule nchini.
Dkt. Komba amesema miongoni mwa matokeo yanayotarajiwa ni kupatikana kwa Azimio la Dar es Salaam kuhusu Mageuzi ya Elimu Barani Afrika, pamoja na kuidhinishwa kwa rasimu ya Mfumo wa Afrika wa Kuandaa na Kuboresha Mitaala (African Continental Curriculum Framework).
Amesema pia kongamano hilo linatarajiwa kutoa mapendekezo ya kisera na kiutendaji kuhusu ujumuishaji wa Akili Unde, zana za kidijitali na maadili ya Kiafrika katika mitaala, huku likiimarisha ushirikiano na ubadilishanaji wa maarifa miongoni mwa wataalamu wa mitaala, watafiti na watunga sera barani Afrika na duniani.
Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Kongamano la ACA 2026 anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratias John Ndejembi, huku Dkt. Komba akiwataka wadau wa elimu kushiriki kikamilifu na wanahabari kusaidia kuifikisha taarifa ya kongamano hilo kwa umma.

