Awataka wasanii kutumia sanaa kutangaza Utalii wa Arusha
Asema Arusha ni Salama, awakaribisha wananchi kupata burudani
Madee, Inspekta Haroun wamshukuru RC Makalla kwa mapokezi yake
Na Mwandishi Maalumu RS Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla amewakaribisha wanamuziki, wasanii na mashabiki wa muziki wa kizazi kipya maarufu kama BongoFleva kwenye Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva, akiwahakikishia usalama kabla, wakati na baada ya Tamasha hilo linalosherehekea safari, Mchango na heshima ya wasanii waliojenga tasnia ya muziki wa kizazi kipya.
Mhe. Makalla ametoa ukaribisho huo leo Ijumaa Septemba 18, 2026 Ofisini kwake Jijini Arusha, alipokutana na kundi la wasanii na waandaaji wa tamasha hilo, wanaotarajiwa kutumbuiza kwenye Tamasha hilo hapo kesho kwenye Viwanja vya General Tyres, akiwataka pia kushiriki katika kutangaza Utalii wa Mkoa wa Arusha kupitia sanaa ya muziki.
Kwa upande wake Hamadi Ally Seneda maarufu kama Madee, Mratibu na muasisi wa Tamasha hilo amemshukuru Mhe. Makalla kwa mapokezi makubwa ya tamasha hilo, akisema kwa hadhi ya Mkoa wa Arusha na namna ambavyo wananchi wake wanapenda Muziki ndiyo sababu ya Uongozi wa tamasha hilo kumchagua msanii wa Kimataifa kutoka Marekani Mr Cheeks kutumbuiza katika tamasha hilo.
Aidha kwa upande wake Haroun Rashid Kahena maarufu kama Inspekta Haroun, kwaniaba ya wasanii wenzake amesema kufanyika kwa tamasha hilo katika Mkoa wa Arusha ni sehemu ya kutoa fursa ya ajira kwa wasanii waliokuwa wamesahaulika, akitoa pia shukrani kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ushirikiano wao mkubwa katika maandalizi ya tamasha hilo

