Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Puma Energy Tanzania imefikia hatua ya kuwa na vituo 100 vya mafuta na huduma za ziada nchini, hatua iliyoadhimishwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo kupitia tukio lililolenga kutambua mchango wao katika mafanikio hayo na kujadili mwelekeo wa ukuaji wa biashara.
Tukio hilo lililofanyika jijini Dar es Salaam, liliwakutanisha wafanyakazi kutoka maeneo na idara mbalimbali za kampuni hiyo kwa lengo la kuimarisha ushirikiano, mshikamano na mahusiano ya kikazi.
Mbali na kusherehekea kufikiwa kwa vituo 100, wafanyakazi walipata fursa ya kutambua juhudi na mchango wa kila idara katika kuhakikisha kampuni inaendelea kukua na kutoa huduma kwa wateja katika maeneo mbalimbali nchini.
Hatua hiyo imekuja wakati Puma Energy Tanzania ikiendelea kutambuliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa nafasi yake katika soko la mafuta nchini, ambapo kampuni hiyo imetajwa kuwa inaongoza kwa ukubwa wa soko kwa miaka minne mfululizo.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma M. Abdallah, alisema kufikisha vituo 100 ni hatua muhimu katika ukuaji wa kampuni, lakini pia ni matokeo ya juhudi na ushirikiano wa wafanyakazi.
Alisema mafanikio hayo yamechangiwa na kujituma kwa wafanyakazi katika maeneo mbalimbali, hivyo tukio hilo lilikuwa fursa ya kutambua mchango wao, kuimarisha mahusiano na kuweka msingi wa hatua zinazofuata katika ukuaji wa kampuni.
“Kufikisha vituo 100 vya mafuta na huduma za ziada ni hatua muhimu katika ukuaji wa biashara yetu, lakini pia ni matokeo ya kazi ya watu walio nyuma ya mafanikio haya,” alisema Abdallah.
Alisema kampuni hiyo inalenga kujenga zaidi juu ya mafanikio yaliyofikiwa, kuimarisha ushirikiano kati ya timu na idara mbalimbali na kuendelea kuwahudumia wateja kwa ufanisi.
Puma Energy Tanzania inaendelea na shughuli mbalimbali katika sekta ya nishati, ikiwemo uendeshaji wa vituo vya mafuta na huduma za ziada, usambazaji wa mafuta, huduma za mafuta ya ndege, vilainishi, pamoja na LPG na lami.
Katika tukio hilo, uongozi pia uliwashirikisha wafanyakazi kuhusu vipaumbele vya biashara kwa kipindi kijacho, hatua iliyowapa nafasi ya kuelewa mwelekeo wa kampuni na nafasi yao katika utekelezaji wa mipango hiyo.
“Tunapoadhimisha kufikisha vituo 100, tunatambua pia kuwa kila hatua ya mafanikio huleta majukumu mapya. Sasa tunalenga kujenga zaidi juu ya tulichokifikia, kuimarisha ushirikiano wetu na kuendelea kuwahudumia wateja kwa ufanisi,” alisema Abdallah.
Aliongeza kuwa wafanyakazi wataendelea kuwa sehemu muhimu ya safari ya Puma Energy Tanzania katika hatua inayofuata ya ukuaji wa kampuni.
Puma Energy ni kampuni ya kimataifa inayotoa huduma za nishati katika nchi zaidi ya 35 duniani, ikiwemo Tanzania, ambako inajihusisha na huduma za mafuta, mafuta ya ndege, vilainishi, LPG na lami.

