NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, amesema maandalizi ya kizazi cha wazalendo yanapaswa kuanza katika ngazi ya awali ya elimu, akisisitiza umuhimu wa kuwapatia watoto elimu na malezi bora tangu wakiwa wadogo.
Ngajilo ameyasema hayo wakati alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa shule ya awali katika Kata ya Makorongoni, Manispaa ya Iringa, unaojengwa kwa nguvu za wananchi pamoja na fedha zilizotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema watoto ndio msingi wa taifa, hivyo jamii inapaswa kuhakikisha wanapata elimu na maarifa mapema ili kuwaandaa kuwa raia wenye uzalendo na mchango katika maendeleo ya nchi.
“Uzalendo unaanzia kwenye ngazi hii ya awali. Hapa ndipo tunapotengeneza taifa,” amesema Ngajilo.
Ameeleza kuwa uzalendo haupaswi kusubiri hadi mtu awe mtu mzima, bali unatakiwa kujengwa hatua kwa hatua kupitia malezi na elimu kuanzia utotoni.
Ngajilo pia ametoa mfano wa ujenzi wa shule za sekondari za kata, akisema wakati wa utekelezaji wa mpango huo kulikuwa na mijadala na ukosoaji kutoka kwa baadhi ya watu waliokuwa wakiona shule hizo zikijengwa kwa kasi wakati changamoto za walimu bado zilikuwepo.
Hata hivyo, amesema kwa sasa shule hizo zimekuwa sehemu muhimu ya mfumo wa elimu na baadhi zimeendelea kufanya vizuri kitaaluma.
Ngajilo ametumia mfano huo kusisitiza umuhimu wa kutekeleza maamuzi ya maendeleo kwa kuangalia mahitaji ya muda mrefu ya taifa, akisema baadhi ya mipango inaweza kuonekana kwa mtazamo tofauti wakati wa utekelezaji lakini baadaye ikaonekana umuhimu wake.
Amesema kuwa atahakikisha anatumia nafasi yake kuyake kuhamisha ujenzi wa shule za awali nchi nzima kuweza kujenga uzalendo tangu awali kama ilivyokuwa ujenzi wa shule za sekondari za kata.
Ujenzi wa shule ya awali Makorongoni ni sehemu ya juhudi za wananchi na Serikali katika kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto katika eneo hilo.

