Afisa mafunzo kutoka Taasisi hiyo ,Abdulwahid Ali Khamis akitoa maelezo kwa Mkuu wa wilaya ya Arusha kuhusu huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo
……….
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha ,Taasisi ya ScanCode Tanzania imesema inatoa huduma mbalimbali za teknolojia kwa wafanyabiashara, wazalishaji na taasisi, ikiwemo matumizi ya barcode na QR Code zinazosaidia kuongeza thamani ya bidhaa na kurahisisha ufuatiliaji wake.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Afisa mafunzo kutoka Taasisi hiyo ,Abdulwahid Ali Khamis wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye kliniki ya viwanda na biashara inayoendelea mkoani Arusha .
Abdulwahid amesema kuwa,wafanyabiashara wanaweza kutumia barcode na QR Code katika bidhaa zao ili kuwasaidia walaji kupata taarifa muhimu kuhusu bidhaa, ikiwemo mzalishaji, aina ya bidhaa na mahali ilikotoka, hivyo kuongeza uwazi na uaminifu kwa wateja.
“ScanCode Tanzania pia imezindua Ubora App, inayopatikana kupitia Play Store na App Store, ambayo inawawezesha watumiaji kuskani barcode au QR Code na kupata taarifa mbalimbali zinazohusiana na bidhaa husika.”amesema .
Amesema kuwa,mbali na huduma hizo, kampuni hiyo inatoa mafunzo kuhusu teknolojia ya Artificial Intelligence (AI) kwa taasisi na wafanyabiashara, ikiwa ni sehemu ya kuwajengea Watanzania uwezo wa kutumia teknolojia hiyo katika kurahisisha shughuli zao na kuongeza ufanisi.
Amefafanua kuwa, mafunzo hayo pia yanalenga kuwasaidia Watanzania kutumia AI kama fursa ya kujipatia kipato, na kusisitiza umuhimu wa jamii kuwa na uelewa wa teknolojia zinazoendelea kukua.
“ScanCode Tanzania ipo Arusha katika Kliniki ya Viwanda na Biashara, na tunatoa elimu na huduma mbalimbali za teknolojia kwa wafanyabiashara na wadau wengine wanaohitaji huduma hizo na natoa wito kwa wafanyabiashara mbalimbali kujitokeza kwa wingi kutembelea banda letu kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali tunazotoza.

